KAIJAGE ASEMA KAMATI ILIKIUKA KATIBA


ALIYEKUWA MSEMAJI WA TFF, FLORIAN KAIJAGE
ALIYEKUWA Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Florian Kaijage, ameibuka na kuishutumu Kamati ya Uchunguzi wa sakata la kugoma kwa CD ya Wimbo wa Taifa wakati wa mchezo wa kimataifa baina ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, na Morocco kwa kudai kuwa imekiuka katiba ya shirikisho hilo katika kufikia uamuzi wake.
Kaijage aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaa leo kwamba kuwa kamati hiyo ilifikia uamuzi wa kummwagia lawama yeye kwamba alizembea ikiwa na wajumbe wawili wakati katiba ya ya TFF inataka maamuzi yoyote yafikiwe na wajumbe wasiopungua nusu ya akidi.
“Ibara ya 36 ya TFF inazungumzia kamati ya utendaji inavyoweza kufikia uamuzi; utafikiwa iwapo akidi itafikia nusu ambapo mara zote lakini mimi nilihojiwa na wajumbe wawili wa kamati hiyo, mwenyekiti na katibu wake jambo ambalo ni ukiukwaji wa katiba,” alisema.
Kaijage alisema ameshangazwa na kamati hiyo kumtupia zigo hilo kwani siku ya tukio fundi mitambo raia wa China mwenye utaalamu wa kuwasha mitambo hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kichina hakuwepo katika eneo lake na kama angekuwepo lisingetokea hilo lakini kamati hiyo kwa sababu zake imeamua kumhukumu yeye.
Aliongeza kuwa siku ya tukio alikuwa na majukumu mengi ikiwa ni pamoja na kushughulikia vitambulisho vya wapiga picha ambao wanaingia eneo la karibu na uwanja, kugawa line- ups na alikuwa akifanya shughuli hizo kwa ushirikiano na ofisa habari aliyeomba TFF, Suleiman Jongo.
Kaijage alisimamishwa na TFF baada ya kutokea kwa tukio hilo la fedheha mbele ya Rais Jakaya Kikwete ili kupisha uchunguzi wa kamati hiyo iliyoundwa na rais wa TFF, Leodgar Tenga, ambayo ilikuwa chini ya mwenyekiti Hamidu Mbwezeleni.
Alisema anaamini siku ya tukio alitimiza majukumu yake na kwa sasa hawezi kuchukua hatua zozote dhidi ya kamati hiyo kwa kuwa si mwajiri wake na TFF haijamchukulia hatua baada ya kupokea ripoti ya kamati hiyo.

Comments