JABULANI IMENIPONZA LUBUMBASHI-KASEJA


NA DINA ISMAIL
WAKATI wapenzi na mashabiki wengi wa soka wakijiuliza maswali mengi kuhusu bao la kwanza ambalo kipa wa Simba, Juma Kaseja alifungwa, kipa huyo ameanika kilichomsibu langoni.
Baada ya mechi ile ya awali ya raundi ya pili iishe kwa Simba kufungwa mabao 3-1, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijiuliza mazingira ya bao lile.
Akizungumza na Sayari, Kaseja alisema shuti lile la Patou Kabangu ambalo lilitokana na mpira wa adhabu, kwanza lilikuwa la kushtukiza mno.
Kaseja alisema, wakati akiwa anapanga mabeki wake vizuri kwa ajili ya adhabu ile, ghafla akashitukia mpira ukielekea katika nyavu.
Mbali ya kupigiwa shuti la kushtukiziwa, Kaseja ambaye ni kipa namba moja wa Simba na timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars alisema, kingine kichompoteza hesabu, ni kuyumba kwa mpira.
“Kulikuwa na mpira wa faulo, hivyo nilipaswa kuwapanga vizuri mabeki wangu, wakati naendelea kupanga ukuta wangu…kumbe mpira ukaanza bila kuona,” alisema Kaseja na kuongeza:
“… Mpira wenyewe ni jabulani, hivyo ulipokuja langoni kwa kushtukiza ukayumba mbele yangu na kutinga wavuni,” alisema na kusisitiza kufungwa huko ni kitu cha kawaida.
Mipira aina ya Jabulani imetengenezwa na kampuni ya Adidas ya Ujerumani ambayo kwa mara ya kwanza kutumika ni katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini kuanzia Juni 11 hadi Julai 11.
Hata katika fainali hizo, mipira hiyo ililalamikiwa na makipa wengi kwamba, ilikuwa ikiyumba ikiwa hewani, hivyo kuwapotesa hesabu katika kuidhibiti.
Mbali ya hilo, Kaseja alisema kama kipa anayepigania ushindi wa timu, hapendi kufungwa iwe amekaa yeye ama kipa mwingine katika lango la timu yake, hivyo amesikitishwa na kipigo cha mabao 3-1.
“Sipendi kufungwa na hata kama sipo mimi langolini, sipendi timu yangu ifungwe…nilijisikia vibaya kupoteza mechi ile (ya TP Mazembe), lakini pamoja na yote, hatuna budi kujipanga
na kwa mechi ya marudiano.
Akienda mbali zaidi, Kaseja alisema anashangazwa na watu kumlaumu kuwa alifungisha mechi ile kitu ambacho hakina ukweli wowote kwani mabao yote yaliingia kutokana na sababu tofauti za kimchezo.
“Mimi ni binadamu kama wengine hivyo kufungwa kule isiwe sababu ya kupakana matope, wanafungwa makocha wa timu kubwa duniani ije kuwa Kaseja.Ifikie wakati Watanzania kuwa wanakubali matokeo”, Aliongeza Kaseja.
Katika mechi hiyo ya ligi ya Mabingwa ya Afrika Simba ililala kwa mabao 3-1 ambapo timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam wiki ijayo.
Mabao mengine ya TP Mazembe, yalifungwa na Amia Ekanga katika dakika ya 27 kabla ya Kaluyituka kupiga la tatu dakika ya 70 kabla ya Okwi kuifungia Simba bao la penati dakika ya 76, hivyo Simba kuwa nyuma kwa mabao 3-1.
Kwa matokeo hayo, Simba inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 katika mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kati ya Aprili 1 hadi 3.

Comments