BONANZA LA WAANDISHI WA HABARI LAHAMISHIWA CINE CLUB

DK. EMMANUEL NCHIMBI, WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO AMBAYE ANATARAJIWA KUWA MGENI RASMI KATIKA BONANZA HILO.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARICHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinawajulisha kuwa kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika sasa tamasha la Media Day Bonanza litafanyika ukumbi wa Cine Club Mikocheni, Dar es Salaam.Tamasha litafanyika kama ilivyopangwa Jumamosi Machi 12, 2011, lakini tumeamua kuhamisha kutoka Coco Beach hadi Cine Club kwa nia ya kulifanya liwe zuri zaidi.Licha ya kuwa malipo yalishafanyika Coco Beach na hata taratibu nyingine za maandalizi zilianza, lakini kumejitokeza jambo lingine kwamba kuna watu wa Tigo wana tamasha lao la mambo ya promosheni siku hiyo.Hivyo kwa kuhofia muingiliano na watu wengine, TASWA pamoja na wadhamini wa bonanza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), leo tulifanya kikao cha dharura na kufikia uamuzi wa kubadili ukumbi.Ingawa Tigo shughuli yao inaanza mchana na ni eneo lile la kuegeshea magari, lakini TASWA na TBL inaona wageni wake watashindwa kujinafasi na kukosa ule uhuru wa kuwa wenyewe kama dhamira ya bonanza ilivyo.Pia tumezingatia maoni ya wadau mbalimbali wa bonanza hili waliotaka tutafute mahali ambapo wataweza kujinafasi zaidi, hivyo TASWA na TBL wanaamini Cine Club ni mahali mwanana.Dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba waandishi 1,000 watakaohudhuria wanakuwa huru bila kuwepo na watu wengine, hivyo TASWA inaomba radhi kwa usumbufu huu, ambao upo katika dhamira ya dhati ya kujenga.Tamasha hili mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, hivyo mambo mengine ikiwemo ratiba inabaki kama ilivyo.Kama tulivyosema jana ni kuwa kesho pamoja na mambo mengine kutakuwa na mashindano ya mbio za meta 100 kwa ajili ya wahariri na mshindi wa kwanza atapewa medali ya dhahabu, wa pili fedha na wa tatu shaba.Michezo mingine itakayoshindaniwa ni soka ya ufukweni (wanaume), netiboli (wanawake), wavu (jinsia zote watachanganyika), mbio za magunia (wanawake na wanaume), mbio meta 100, kuruka kichura (wanawake na wanaume) na kuvuta kamba (jinsia zote watachanganyika) na kucheza muziki (wanawake na wanaume).
Amir Mhando
Katibu Mkuu

Comments