ZAWADI KIBAO BONANZA LA WAANDISHI WA HABARI JUMAMOSI



KAMPUNI ya Airtel imetangaza rasmi zawadi za washindi wa michezo mbalimbali zitakazotolewa katika Tamasha la Wanahabari linalotarajiwa kufanyika keshokutwa Jumamosi kwenye viwanja vya TTCL Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Muganyizi Mutta alisema, wameandaa zawadi hizo kwa ajili ya kuongeza hamasa ya ushindani miongoni mwa vyombo vya habari vitakavyoshiriki tamasha hilo.
Mutta alizitaja zawadi hizo kuwa ni pamoja na mataji yenye thamani ya sh milioni 6 kwa washindi wa soka, netiboli, kuvuta kamba, kucheza dansi na kuimba, ambako pia kutakuwa na zawadi za papo kwa papo kwa michezo mbalimbali ya kubahatisha itakayochezeshwa na kampuni hiyo.

“Tumeandaa zawadi mbalimbali za kuvutia, katika kuongeza hamasa na ushindani kwa washiriki, lakini pamoja na hilo kutakuwa na zawadi za promosheni kwa michezo tofauti ya kubahatisha itakayochezwa na Airtel, ili washiriki waweze kuburudika kwa kiwango chake,” alisema Mutta.

Comments