YANGA YADAI PAPIC KATOROKA NA MAMILIONI


UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema kuwa aliyekuwa kocha wake mkuu Kostadin Papic ametoroka na mamilioni ya fedha za klabu hiyo hivyo wanafanya taratibu za kisheria ili kumpata.
Papic alitoroka nchini juzi kwenda kwao Serbia, huku uongozi wa timu hiyo ukisema kwamba hatoweza kuondoka mpaka pale atakapojibu shutuma mbalimbali zinazomkabili.

Mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba kocha huyo aliamua kujiuzuru na kabla ya kutoroka baada ya kuona huenda aliyoyafanya yataweza kumletea matatizo.

Alisema Papic alifanya usajili wenye utata kwa kuwalipa wachezaji fedha pungufu za usajili wakati hela zote zilitolewa,huku akimtolea mfano Omega Seme ambaye alimpatia milioni 10 badala ya 15 zilizotolewa.

Nchunga pia alisema kocha huyo alichakachua fedha za usajili wa Mghana Kenneth Assamoh kwa kuidanganya klabu aliyotoka kuwa Yanga imesajili kwa mkopo wakati fedha za usajili wake zilitolewa.

Kama hiyo haitoshi, Papic alitumia hela za kumsajili kipa kutoka Serbia Ivan Knezevic, huku pia akiondoka na dola 3,000 alizokopa mwezi Agosti mwaka jana.

“Tutamfuatilia kwa namna moja ama nyingine yeye pamoja na wengine wanaohusika katika sakata hili tutawachukulia hatua za kisheria”, Alisema Nchunga.
Hata hivyo habari zilizopatikana jana zinadai kuwa mmoja ya viongozi wa Yanga anahusika katika mchakato wa kumtorosha Papic.

Comments