YANGA WAFANYIWA HUJUMA ETHIOPIA


SIKU moja kabla ya kushuka dimbani kuwakabili Dedebit ya Ethiopia katika mechi ya marejeano, wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Yanga ya jijini Dar es Salaam imekiona cha moto baada ya kugandishwa uwanja wa ndege wa Addis Ababa Ethiopia kwa takriban saa nne alfajiri ya jana mara walipowasili.
Akizungumza kwa simu kutoka Ethiopia jana, msemaji wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kwamba mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege walijikuta wakiganda kwa zaidi ya saa nne, kutokana na wenyeji wao kutofika kuwapokea na kuwapeleka katika hoteli.
Alisema, walifika majira ya saa 12:30 alfajiri ya jana, lakini cha kushangaza walikaa uwanjani hapo hadi saa 4:30 asubuhi, ndipo walipokuja wawakilishi wa timu hiyo na kuwapeleka katika hoteli.
Kama hiyo haitoshi, Sendeu alisema hata hoteli waliyopelekwa iitwayo Ras, ilikuwa haina sifa zinazostahili, lakini pamoja na kulalamika wenyeji wao hao waliwaeleza kwamba haitowezekana kuwatafutia mahala pengine, kwani timu zote huwa zinafikishiwa hapo.
Sendeu aliongeza kuwa hali hiyo ilimfanya balozi mdogo wa Tanzania nchini humo, Vicent Kibwana, kuingilia kati na kuzungumza na wachezaji, hivyo kulimaliza tatizo hilo.
“Balozi alitueleza kuwa hali ile ni njama za kutaka kutuvunja moyo ili tufanye vibaya katika mechi yetu…tulirudisha mioyo nyuma na kuendelea kukaa hotelini hapo,” alisema Sendeu.
Sendeu aliongeza kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri na jana jioni walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis watakaochezea.
Yanga iliondoka usiku wa kuamkia jana, huku kocha wake mkuu, Sam Timbe, akiwa na matumaini ya kikosi chake kurejea na ushindi katika mechi yake hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Timbe alisema siku chache alizokuwa na timu hiyo, amezitumia kurekebisha mapungufu aliyoyaona tangu alipowasili ambayo anaamini yatasaidia kushinda mechi hiyo.
Alisema, matumaini ya timu yake kushinda yanatokana na kiwango walichonacho wachezaji wake, akilinganisha na wapinzani wao, baada ya kuwaona katika mechi yao ya awali iliyopigwa jijini Dar es Salaam.
“Niliiona mechi ya awali kabla sijajiunga na Yanga, hivyo mapungufu ya timu yangu nimeyafanyia kazi na yale ya wapinzani wetu pia tumeyafanyia kazi, nadhani vijana hawataniangusha siku hiyo,” alisema Timbe.

Comments