UKATA WAIKWAMISHA TIMU YA TAIFA YA TENISI KWENDA MOMBASA


Na Samia Mussa
TIMU ya taifa ya tenisi Tanzania imeshindwa kushiriki mashindano ya vijana chini ya miaka 18 yanayotarajiwa kufanyika Februari 26 Mombasa nchini Kenya.

Kocha wa mchezo huo, Salum Mvita, alisema kuwa wameshindwa kuthibitisha kushiriki mashindano hayo kwa sababu ya ukata unaokikabili Chama cha Tenisi Tanzania (TTA).
Alisema kuwa kutokana na kupata taarifa za pamoja za mashindano ya Nairobi kwa vijana chini ya miaka 14 na ya Mombasa chini ya miaka ya 18, kumewafanya washindwe kujiandaa kwa mashindano hayo, kwa sababu ya kutokuwa na fedha, hivyo kuamua kujiandaa na mashindano ya Nairobi.
Alisema, ni fedha nyingi zinatakiwa kujiandaa na mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na dola 70 kwa kila mchezaji anayetaka kujiunga katika mashindano hayo, ambako hata akitokea mdhamini wa kusaidia hawataweza kushiriki kwa sababu muda wa maandalizi umemalizika.
Mashindano hayo pamoja ya Nairobi yanayotarajia kufanyika Aprili 4, yameandaliwa na Chama cha Tenisi Kenya (KTA), kwa kushirikiana na Shirikisho la Tenisi la Kimataifa (ITF).

Comments