TIMU YA SOKA YA VIJANA CHINI YA MIAKA 23 YATANGAZWA

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ jana alitangaza nyota wake 25 watakaoshiriki mashindano ya mchujo ya Olimpiki, Machi 26 dhidi ya Cameroon jijini Younde.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Julio alisema, timu hiyo inaanza mazoezi leo asubuhi Uwanja wa Karume, kabla ya kambi inayotarajiwa kuanza Februari 26.
Alisema, watacheza michezo miwili ya kirafiki kati ya Machi 12 hadi 20, kabla ya Machi 22 kwenda Cameroon.
Pia alibainisha kuwa kikosi alichokichagua kinatarajia pia kuiwakilisha Tanzania katika mashindano mengine ya kimataifa, kutokana na kushirikisha vijana wa kati miaka 17-20.
Aliwataja nyota wanaounda kikosi hicho kuwa ni pamoja na makipa Shabani Kado (Mtibwa), Salehe Malande (TSA), na Daud Gabriel (Azam FC), wakati mabeki wa pembeni ni Salum Telela (Yanga), Hassan Kessy na Issa Rashid (Mtibwa/TSA).
Mabeki wa kati ni Zahoro Pazi (African Lyon), Mbwana Hamis (Simba), Louis Tumba, Omar Mtaki (Azam), na Babu Ally (Morani Fc).
Viungo ni Godfrey Innocent (Simba) Salum Abubakar, Ibrahim Juma, Himid Mao (Azam), Samwel Ngassa (African Lyon), Omega Seme (Yanga), na Frank Damayo (JKT Ruvu).
Viungo wa pembeni ni Jamal Mnyate, Cosmas Freddy (Azam), na Edward Shija (Simba), huku washambuliaji ni Benedict Ngassa (Moro United), Atupele Green (Yanga), Mbwana Samata (Simba), na Thomas Ulimwengu (TSA).

Comments