TASWA YAMPONGEZA LEODGER TENGA


TENGA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinatoa pongezi kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodeger Tenga kuchaguliwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF baada ya kumshinda Celestine Musabiyima wa Rwanda aliyekuwa akitetea nafasi hiyo uchaguzi uliofanyika Khartoum, Sudan.
TASWA inaungana na wadau wa soka pamoja na wapenda michezo wengine wote Tanzania kumtakia kila la kheri Tenga, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika wadhifa wake huo mpya, huku tukiamini utakuwa na manufaa kwa soka letu na ukanda huu kwa ujumla.
Licha ya kumpongeza, lakini tunampa changamoto aelewe kwamba kutekeleza na kutelekeza ni maneno mawili yanayoshabihiana katika kuyatamka na usipokuwa makini yanaweza kukuchanganya na kukupoteza kabisa.
Lakini haya ni maneno yenye maana tofauti, ambazo moja ni kama chanya na nyingine hasi. Neno kutekeleza maana yake kwa tafsiri rahisi ni kufanya, wakati kutelekeza maana yake ni kutofanya, kuacha au kupuuzia.
TASWA inaamini Tenga atatekeleza mambo mbalimbali, ambayo yalimsukuma kuwania wadhifa huo na hatayatelekeza.
Kama ataona kuna mambo magumu asiwe mvivu wa kuomba ushauri kwa Mtanzania mwingine aliyepata kushika wadhifa huo, Said Hamad El Maamry ambaye aliwahi kushinda nafasi hiyo mwanzoni mwa miaka ya 80 kwa vipindi viwili mfululizo.
Ahsante,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
25/02/2011

Comments