TASWA YAANDAA MECHI KUCHANGIA WODI YA WAZAZI HOSPITALI YA MKURANGA

AMIR MHANDO, KATIBU MKUU WA TASWA
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa mchezo maalum wa soka kati ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2010/2011 na timu ya wachezaji nyota 16 wa ligi hiyo.

Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando, amesema kwamba mchezo huo utafanyika Aprili 16 mwaka huu,Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Alisema wamekubaliana kuwa asilimia kumi ya mapato ya mchezo huo yatapelekwa kwenye wodi ya wazazi ya hospitali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

“TASWA kama wadau wakubwa wa michezo tumeona ni vyema nasi tushirikiane na jamii katika masuala ambayo yatakuwa na msaada mkubwa, hivyo kwa kuanzia tumeamua kuandaa mchezo huu.

“Tunaamini utakuwa mchezo mzuri, kwani wachezaji hao nyota 16 watatoka timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom na timu itaitwa Vodacom All Stars,” alisema Mhando.

Alisema kamati ya Utendaji ya TASWA imewateua wanachama wake wawili ambao wana taaluma ya ukocha Ally Mkongwe na Ibrahim Masoud kusimamia timu hiyo.

Alisema Masoud na Mkongwe ndiyo watakuwa na jukumu la kutafuta wachezaji bora hao 16 kwa ajili ya timu hiyo na kuwa wanatakiwa wakamilishe kazi hiyo Machi 30 mwaka huu, ambapo Ligi Kuu itamalizika Aprili 10.

Aprili mwaka juzi TASWA iliwahi kuandaa mchezo wa hisani kati ya Simba na timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ ambao ulikuwa maalum kupinga
mauaji dhidi ya albino.

Kabla ya mchezo wa Simba Zanzibar Heroes ambao ulifanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kulifanyika mchezo wa utangulizi kati ya TASWA FC na timu ya albino.

Comments