TAKUKURU YAKOMAA NA MWAKALEBELA


MWAKALEBELA AKIWA NA MKEWE SELINA MWAKALEBELA AMBAPO KESHO WATAPANDA KIZIMBANI MJINI MBEYA KWA KESI NYINGINE INAYOWAKABILI.
Na Francis Godwin, Iringa
SIKU moja baada ya mahakama ya hakimu mkazi wa wilaya ya Iringa kumwachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Frederick Mwakalebela, katika shtaka lake la rushwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Iringa mjini, taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Iringa, imekusudia kuendelea na kesi hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima, juzi, mwanasheria wa Takukuru mkoani Iringa, Ntimu Mizizi, alisema kuwa maamuzi ya mahakama hiyo chini ya hakimu Festo Lwila ameyakubali na kuwa mapungufu yaliyokuwemo awali katika kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2010 taasisi hiyo inayafanyia kazi na kufungua kesi yenye maelekezo ya mahakama.
Alisema kuwa maamuzi ya mahakama katika kesi hiyo yameonekana ni mazuri na yenye maelekezo ya kina zaidi kuliko ilivyokuwa kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai kwani mahakama haikwenda kiundani zaidi kama ilivyo katika maamuzi madogo ya kesi ya Mwakalebela.
Hata hivyo, alisema kuwa leo kutakuwa na majibu sahihi dhidi ya uamuzi wa Takukuru katika kuendelea na kesi hiyo ama la.
“Nakuomba unitafute Jumatatu; nitakuwa na majibu sahihi ….japo maandalizi ya shtaka jipya yatakuwa yamefanyika,” alisema.
Mahakama hiyo chini ya hakimu Lwila ambaye alikuwa anasikiliza shauri hilo, aliindoa kesi hiyo na kumwachia huru Mwakalebela baada ya kuridhika na hoja moja ya upande wa utetezi kwamba kulikuwa na mapungufu ya kisheria kwenye hati ya mashtaka.
Mapungufu hayo ni mtuhumiwa kushtakiwa kwa makosa mawili kwenye hati moja ya mashtaka na hivyo kumfanya mtuhumiwa ashindwe kuelewa kwa usahihi kosa linalomkabili kitu ambacho kinaweza kumfanya ashindwe kuandaa utetezi wake.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Basil Mkwata wa Mkwata
Law Chambers, uliwasilisha pingamizi la awali la kisheria ambalo lilikuwa na hoja tatu.
Hata hivyo Mwakalebela leo atapanda kizimbani kuendelea na kesi nyingine namba 8 ya mwaka 2010 ambayo inamkabili yeye pamoja na mkewe, Selina, ambayo iko hatua ya kutolea hukumu pingamizi la kisheria iwapo iondolewe mahakamani au la.

Comments