SIMBA KUPIGA KAMBI ARUSHA AMA NAIROBI


KIKOSI CHA SIMBA

KATIKA kujiandaa na mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, wawakilishi wa Tanzania Simba ya jijini Dar es Salaam imepanga kupiga kambi katika miji ya Arusha ama jirani Nairobi Kenya.
Hatua hiyo, inatokana na kubanwa na ratiba ya ligi kuu bara, hivyo kuamua kuahirisha mipango yao ya awali.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, wataweka kambi katika miji hiyo kutokana na hali ya hewa kufanana na ile ya Lubumbashi, DRC nyumbani kwa TP Mazembe.
Alisema, wameona timu yao ijifue katika miji hiyo kabla ya kwenda DRC, kwani watakipiga na AFC ya Arusha Machi 12, hivyo kuwa na muda mfupi wa kujiandaa zaidi.
“Kambi yetu ya nje kwa kweli ni vigumu kwa sasa kutoka nje ya nchi, kwani ratiba ya ligi inatubana, Jumapili tunacheza na Mtibwa, kisha Machi 5 na Yanga, halafu AFC, sasa ni bora siku hizo tuangalie kama kubaki Arusha ama Nairobi,” alisema Kaburu.

Comments