SHIBOLI ALIA NA POULSEN

ALI AHMED SHIBOLI

MSHAMBULIAJI wa Simba, Ali Ahmed Shiboli amesema kupangwa dakika tano katika mechi hakuwezi kudhihirisha ubora alionao mchezaji.
Hatua hiyo inafuatia kutemwa kwake katika kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kitakachocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya
Palestina katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma jana, Shiboli alisema hajisikii vibaya kuachwa kwani hata alipokuwepo, hakupewa nafasi ya kutosha kuonyesha uwezo wake halisi.
Alisema katika hali ya kawaida, huwezi kukiona kiwango halisi cha mchezaji ndani ya dakika tano alizokuwa akipewa na Kocha wa Stars, Jan Poulsen.
“Tunarudishana nyuma kwa kweli kwani sikupewa nafasi ya kuonyesha kiwango changu halisi, dakika tano haziwezi kuonyesha kiwango cha mtu, lakini huwezi kupingana na uamuzi wa kocha,” alisema.
Shiboli ambaye ni mfungaji bora mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya Zanzibar, alisema kwa sasa anaendelea vema na timu yake ya Simba ambayo ipo katika harakati za kutetea ubingwa.
Kabla ya kujiunga Simba, Shiboli alisajiliwa na KMKM ya Zanzibar ambapo hata hivyo hakuichezea, ilipomnyakua kutoka Mundu Fc ya visiwani humo.

Comments