PAPIC ATOROKA YANGA

PAPIC
NI kama mchezo wa kuigiza vile, kwani wakati jana uongozi wa Yanga ulidai kuwa kocha mkuu wa timu hiyo KOstadin Papic hawezi kuondoka mpaka pale atakapojibu baadhi ya shutuma zinazomkabili, lakini jana hiyo kocha huyo alipanda ndege na kwenda kwao Serbia.

Papic ambaye aliyekatisha mkataba wa kuinoa klabu hiyo, alitoa masharti magumu ya kuendelea kuinoa timu hiyo kama mbinu ya kutimkia, alitakiwa kutoa ufanuzi wa fedha za usajili.
Hiyo inatokana na Papic aliyekatisha mkataba wa kuinoa timu hiyo akipinga kuchomekewa Msaidizi Fred Felic Minziro, kutakiwa kutoa kwanza ufafanuzi wa baadhi ya mambo.
Habari zilizopatikana jana kutoka Yanga zinasema, uongozi wa Yanga umemtaka Papic atoe maelezo na uthibitisho wa nyaraka wa usajili wa wachezaji akiwemo Keneth Asamoah aliyeishia benchi kwa kukosa kibalki cha uhaimisho wa kimataifa (ITC).
Mbali ya kutaka kumbana kuhusu hilo, pia Yanga inataka Papic aendelee na kazi yake kwani alitoa notisi ya siku 30 ya kuacha kazi wakati tayari akiwa amelipwa mshahara wa hadi Februari 15.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya klabu ya Yanga, kinasema kuwa hadi muda huo Papic ameshalipwa kiasi cha 12,835,000.
“Kwa maana hiyo, Papic hawezi kuondoka kwa sasa kwani yeye bado ni mwajiriwa wa Yanga na ameshachukua mshahara hadi wa Februari 15,” kilisemna chanzo hicho.
Chanzo hicho kilionyesha kushangazwa na kocha Papic kushindwa kukaa katika benchi la Yanga siku ilipokwaana na Dedebit ya Ethiopia kwa sababu mkataba bado unamtambua.
“Tunasikia anataka kuondoka, lakini kwa mazingira yaliyopo Papic hawezi kuondoka kwa sababu kama amevunja mkataba na Yanga, alipaswa kurejesha fedha ya hadi Februari 15 alichukua,” kilisisitiza chanzo hicho na kuongeza:
“Kuna mambo kama matatu hivi ambayo Papic anapaswa kutupatia maelezo ya kuridhisha, vinginevyo hawezi kuondoka nchini labda ‘apae kwa ungo,’ wengi hawajui kinachoendelea, kuna mambo anatakiwa kuyajibu kwanza,” kilisema chanzo hicho.
Kati ya mambo hayo ni Papic kueleza vipi Yanga ilisajili kwa gharama kubwa wachezaji wa kimataifa kama Kenneth Assamoh na wengine, lakini wakiishia benchi.
Aidha, Papic ametakiwa kabla hajaondoka nchini aeleza utata wa usajili wa kipa Mserbia, Ivan Knezevic na deni lake la kiasi cha shilingi mil 3.7 ambazo alizikopa tangu Agosti 2010.
“Kwa mfano kipa Mserbia, ameshindwa kuonyesha kiwango kama Papic alivyokuwa anadai...usajili wa huyu ulifanya kutemwa kwa Marashi (Steven) ambaye kiuchezaji, ni mzuri kulikoa huyo Mserbia,” kiliongeza chanzo hicho.
Aidha, kocha huyo ametakiwa atoe ufafanuzi wa fedha za usajili wa kila mchezaji na uthibitisho wake kuwa alichukua kiasi gani na nini kimebaki kwa sababu suala hilo lilikuwa chini ya kocha huyo kwa asilimi 100.
Tangu Kamati ya Utendaji ya Yanga imwidhinishe Minziro kuwa Kocha Msaidizi, Papic amesusa kuifundisha timu hiyo akisema si chaguo lake, hivyo amekuwa akitaka kulipwa stahili zake.
Wakati akijenga hoja ya kutaka kupewa chake, habari zinasema uongozi wa Yanga umemgeuka na kumtaka asiondoke hadi atakapotoa maelezo ya kina kuhusu utata wa usajili wa wachezaji.

MWENYEKITI WA YANGA LLOYD NCHUNGA AMESEMA KOCHA HUYO AMEWATOROKA NA WATAFANYA JITIHADA ZA KUMTAFUTA ILI AWEZE KUJIBU MAELEZO ALIYOTAKIWA KUYATOA.

Comments