LEODGER TENGA AKWAA UJUMBE CAF


LEODGER TENGA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika uchaguzi uliofanyika leo jijini Khartoum, Sudan.
Tenga aliyekuwa akigombea kupitia Kanda ya Mashariki na Kati alimshinda Celestine Musabiyima wa Rwanda aliyekuwa akitetea nafasi hiyo. Tenga ambaye ni Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) alipata kura 34 dhidi ya 19 za mpinzani wake.
Anakuwa Mtanzania wa pili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF baada ya Said Hamad El Maamry ambaye aliwahi kushinda nafasi hiyo mwanzoni mwa miaka ya 80 kwa vipindi viwili mfululizo.
Alishindwa kutetea nafasi hiyo katika kipindi cha tatu baada ya TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu (FAT) kutoidhinisha jina lake CAF. El Maamry hivi sasa ni mjumbe wa heshima wa CAF.
Mtanzania mwengine aliyewahi kuwania nafasi hiyo mara mbili, lakini hakufanikiwa kushinda ni Muhidin Ndolanga ambaye aliwania wakati huo akiwa Mwenyekiti wa FAT.
Kalusha Bwalya naye amefanikiwa kwa mara ya kwanza kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF baada ya kuchaguliwa jana akiwakilisha Kanda ya Kusini mwa Afrika. Bwalya ambaye alikuwa mwanasoka bora wa Afrika mwaka 1988 aliwashinda wagombea wengine wanne.
Aliwashinda Adam Mthethwa wa Swaziland, Walter Nyamilandu (Malawi), John Muinjo (Namibia) na Justino Fernandes wa Angola.
Nafasi ya Kanda ya Magharibi mwa Afrika ilitwaliwa na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Comments