BILIONI 63 ZAHITAJIKA KUFUFUA TRC

ISMAIL ADEN RAGE, MBUNGE WA TABORA MJINI
Na Waandishi Wetu, Dodoma
JUMLA ya sh bilioni 63 zinahitajika ili kulifufua upya Shirika la Reli nchini (TRC) na kurejesha ufanisi wake, imeelezwa.

Akizungumza hayo, Waziri wa Uchukuzi Injinia Omary Nundu alisema hivi sasa TRC ipo taabani kiasi cha kufanya safari moja kwa wiki reli ya kati huku kukiwa hakuna uhakika wa safari hizo wakati mwingine.

Waziri huyo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Ismail Aden Rage(CCM) ambaye pamoja na mambo mengine alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuhakikisha shirika hilo la umma linaimarika na kuendelea kutoa huduma kama zamani.

Injinia Nundu alisema hivi sasa serikali ipo katika hatua za mwisho za kuvunja mkataba kati yake na kampuni ya RITES ya India na tayari imeunda menejimenti ya mpito inayoongoza shirika hilo analokiri kufa kiutendaji baada ya kuingia ubia na Rites.

Alisema mkakati wa sasa wa shirika hilo ni kuongeza safari za treni toka safari mbili za treni zilizokuwepo Desemba, 2010 hadi safari tatu Juni mwaka huu na safari tano itakapofika mwishoni wa mwaka.

Alisema hadi sasa reli ya kati inahudumia zaidi ya wakazi 10,000 wakutoka katika mikoa iliyopo pembezoni mwa reli ya kati na mikoa ya kanda ya ziwa.

Waziri alisema kuwa awali serikali iliingia ubia na muwekezaji huyo wakiwa na idadi ya hisa 49 za serikali dhidi ya hisa 51 za mwekezaji na kuongeza kwamba licha ya kuwa na idadi hiyo ya hisa lakini halikuweza kuendele mbele na hatimaye kufa.

Katika swali la msingi ambalo liliulizwa na Muhonga Ruhanywa kwa niaba ya Mbunge mwenzake wa Mpanda Mjini Said Arfi (CHADEMA) aliyetaka kujua ni lini usafiri na huduma za gari moshi zitarudi kwenye utartibu wake.

Comments