BANKA, MGOSI WAREJESHWA STARS, SHIBOLI, TEGETE NJE

KUTOKA KUSHOTO KASEJA, MGOSI NA BANKA WOTE WAMEITWA STARS
KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenish Jan Poulsen jana ametaja kikosi chake kitakachokipiga na Palestina Februari 9 jijini Dar es Salaam huku akiwarudisha kundini nyota wake wanne na wengine wapya wanne.
Kwa mujibu wa Poulsen, nyota hao saba wamerejeshwa kutokana na kuonyesha uwezo katika mechi kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara hatua ya pili iliyoanza Januari 15.
Akizungumzia umuhimu wa mechi hiyo ya kirafiki, Poulsen alisema ni kipimo kizuri, ingawa Stars iko nafasi ya 117 kwa ubora duniani huku Palestina ikiwa ya 127.
Waliorejeshwa ni Mussa Hassan Mgosi, Mohamed Banka na Juma Jabu ( Simba); na Godfrey Bonny wa Yanga.
Wapya ni Chacha Marwa wa Yanga, Mbwana Samata kutoka Simba, Julius Mrope anayekipiga Mtibwa Sugar na Ramadhan Chombo ‘Redondo,’ wa Azam FC.
Waliosalia ni makipa Juma Kaseja (Simba) na Shaban Kado (Mtibwa Sugar).
Mabeki: Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub ‘Canavaro’ (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Haruna Shamte na Juma Jabu (Simba).
Viungo: Shaban Nditi (Mtibwa Sugar), Nurdin Bakari (Yanga), Jabir Aziz (Azam).
Washambuliaji: Mrisho Ngassa, John Bocco (Azam FC), Machaku Salum (Mtibwa Sugar).
Mechi hiyo kwa Stars ni sehemu ya maandalizi ya kutafuta nafasi ya kushiriki fainali za kombe la Afrika (CAN) mwaka 2012 Guinea ya Ikweta na Gabon.
Katika kundi lake la nne, Stars yenye pointi moja inakamata nafasi ya tatu nyuma ya vinara Afrika ya Kati na Morocco iliyo nafasi ya pili huku Algeria ikiwa ya mwisho.
Mechi hiyo ni muhimu kwa Stars kwa ajili ya kusaka makali ya kuwakabili Afrika ya Kati, mechi itakayopigwa nchini kati ya Machi 25 na 27.

Comments