VILABU VYA LIGI KUU RUKSA KUTUMIA UWANJA WA TAIFA


SERIKALI imeruhusu timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kuutumia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Januari 15, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya Uwanja wa Uhuru kufungwa kutokana na matengenezo.
Alisema hatua ya kuruhusiwa kuutumia Uwanja wa Taifa, imefikiwa jana baada ya kikao kati ya TFF na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Kabla ya serikali kuruhusu kuutumia Uwanja wa Taifa, michezo ya Ligi Kuu ilikuwa ikichezwa Uwanja wa Uhuru ambao ulifungwa kupisha matengenezo madogo kwa ajili ya kumuapisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Pamoja na suala hilo la kuapishwa katika uwanja huo, lakini serikali imeufunga tena uwanja huo kwa ajili ya matengenezo ya majukwaa uwanjani hapo.
Kwa uamuzi huo wa serikali, sasa kuna uwezekano mkubwa kwa Simba na Yanga ambazo zilikuwa zimechagua viwanja vya CCM Kirumba na Jamhuri Morogoro kurejea jijini ikiwamo mechi yao ya Machi 5.

Comments