STARS KUTUPA KARATA YA PILI KESHO DHIDI YA BURUNDI

TIMU ya Taifa ya soka Tanzania ‘Taifa Stars’ kesho inashuka dimbani jijini Cairo Misri kujiuliza na majeruhi mwenzake Burundi ‘Indamba Murugamba’ katika michuano ya nchi za ukanda wa bonde la Mto Nile ‘Nile Basin’ inayondelea nchini humo.
Stars na Indamba zote zinashuka dimbani zikiwa na kumbukumbu ya vichapo katika mechi zao za kwanza, ambako Tanzania ililala 5-1 mbele ya wenyeji Misri ‘Pharaos’ huku Burundi ikipokea kipigo cha 3-1 kutoka kwa Uganda ‘The Cranes’.
Stars baada ya kipigo hicho cha 5-1, Kocha mkuu wake, Mdenish Jan Poulsen alisema kimewapa fundisho kwa kuwa walicheza na timu bora barani Afrika ambayo ni ya kwanza kwa ubora barani Afrika huku Tanzania ikishika nafasi ya 27 kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Tayari kocha Poulsen amesema anatarajia kusahihisha makosa yaliyofanywa na timu yake katika mechi dhidi ya Misri kwa kuchukua pointi tatu muhimu dhidi ya Burundi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa kombe hilo.

Mechi ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani kutokana Stars kutaka kuendeleza ubabe wa kuifunga Burundi huku nao wakitaka kufuta uteja, baada ya kutandikwa na Stars mabao 2-0 wakati wa mashindano ya Tusker Chalenji Cup hivi karibuni , yakipachikwa wavuni na mshambuliaji wake Nurdin Bakari.
Stars ili iweke hai matumaini ya kufuzu nusu fainali italazimika kushinda mchezo wa leo na kusubiri mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda.
Michuano hiyo inashirikisha timu saba zilizogawanywa katika makundi mawili, ambapo timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tatu kila kundi zitacheza kuwania mshindi wa tano. Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya sh. Milioni 200 za Tanzania.

Comments