KIPIGO CHA MAFARAO CHAMCHANGANYA KOCHA TAIFA STARS


Na Mwandishi Wetu, Cairo

KIPIGO cha mabao 5-1 ilichokipata Taifa Stars juzi kutoka kwa Misri kimemchanganya Kocha Jan Poulsen, lakini akisema wamejifunza na watasahihisha makosa yao.

Akizungumza baada ya mchezo baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Arab Contractors mjini hapa, Poulsen raia wa Denmark, alisema Stars ilifungwa na timu bora Afrika.

“Tumecheza na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi ya 116 tuliyopo Tanzania na wao wapo katika 20 bora za dunia, pia ndiyo namba moja Afrika.

“Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri,ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika,” alisema Poulsen.

Kocha huyo alieleza kuwa makosa machache waliyoyafanya wachezaji wake yalitumiwa vizuri na wapinzani wao kufunga na hiyo ilitokana na kucheza bila kuelewana dakika 20 za mwanzo.

“Watanzania tumejifunza mengi kwa mechi ya leo (juzi), faida yake itaonekana mechi zijazo,” alisema Poulsen.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Misri, Hassan Shehata aliisifu Stars na kusema inahitaji marekebisho kidogo lakini itakuwa nzuri.

Alisema mpira ambao Stars ilicheza kipindi cha pili, kama ingecheza hivyo kipindi cha kwanza mchezo ungekuwa mgumu kwao na kusisitiza kuwa timu yake licha ya kupata ushindi mnono, lakini ilikabiliana na upinzani mkubwa.

Kwa upande wake, nahodha wa Stars, Nsajigwa Shadrack alisema hali ya hewa ya baridi kali nayo iliwachanganya kiasi fulani wachezaji hasa kipindi cha kwanza,lakini baadaye walichangamka wakati tayari mambo yameharibika.

Aliwaomba Watanzania wasikatishwe tama na matokeo hayo na kukumbusha kuwa hata michuano ya Chalenji iliyomalizika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Zambia lakini ikaja kuibuka bingwa.

Naye nahodha wa Misri, Wael Goma alisema michuano hiyo ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ni migumu na kwamba Tanzania si timu ya kubezwa, kwani ina wachezaji wenye miili midogo, lakini wana vipaji.

Taifa Stars juzi ilikubali kipigo hicho, ambapo bao la kwanza lilifungwa na Said Khamdi dakika ya nne, kisha dakika kumi baadaye Mohammed Aboutrika alifunga la pili na dakika tisa baadaye beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akajifunga.

Bao la nne lilifungwa na Said Khamdi dakika ya 57, wakati lile la mwisho lilifungwa na Ahmed Ally dakika ya 74 na la Stars lilifungwa na mchezaji aliyetokea rizavu Rashid Gumbo dakika ya 77.

Kesho Stars itacheza na Burundi ambayo nayo juzi ilifungwa mabao 3-1 na Uganda, hivyo ili Stars iweke hai matumaini ya kufuzu nusu fainali italazimika kushinda na kusubiri mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda.

Michuano hiyo inashirikisha timu saba zilizogawanywa katika makundi mawili, ambapo timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tatu kila kundi zitacheza kuwania mshindi wa tano. Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya sh. Milioni 200 za Tanzania.

Comments