KASEJA AOMBA RADHI KWA KIPIGO CHA MABAO 3-2 DHIDI YA AZAM FC


KIPA wa Simba Juma Kaseja amewaomba radhi wanachama, wapenzi na mashabiki wa Simba kutokana na kipigo ilichokipata Simba cha mabao 3-2 kutoka kwa Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu ya Bara iliyochezwa jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kaseja, kipa namba moja wa Simba na timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, aliyasema hayo baada ya Tanzania Daima kutaka maoni yake kuhusu kipigo hicho kilichowanyima mabingwa hao watetezi pointi tatu.
Wakati na baada ya mechi hiyo, wapenzi na mashabiki wa Simba wameonekana kuelekeza lawama kwa Kaseja kwamba uzembe wake uliigharimu Simba.
Kaseja kwa upande wake amewaomba radhi wanachama, wapenzi na mashabiki ambao wameumizwa na kipigo akisema soka ni mcgezo wa makosa, hivyo kwa bahati mbaya, juzi ilikuwa upande wa Simba.
Alisema kipigo kutoka kwa Azam FC, kimemuumiza na kumsikitisha mno, lakini wapenzi na amshabiki wakumbuke katika soka kuna matokeo ya aina tatu ambayo ni kushinda, kufungwa ay sare.
“Imeniuma sana kufungwa na Azam, lakini ndiyo sehemu ya mchezo, hivyo iwe changamoto kwetu ya kurekebisha makosa ili tufanye vema katika mechi zinazofuata,” alisema.
Kaseja aliongeza kuwa, mabao aliyofungwa juzi, yamekuwa funzo kubwa kwake kwani kuanzia sasa atalazimika kuwa makini zaidi katika mechi zijazo kwenye kampeni ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo.
Juzi, Azam juzi walifanikiwa kulipa kisasi cha kufungwa na Simba mabao 2-1 katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.Katika hatua nyingine Simba inatarajiwa kuondoka kesho kwenda nchini Comoro tayari kwa mechi yake ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Elan Club ya mjini Mitsoudje.

Comments