KASEJA ACHEKELEA KUITOA TKO TFF

JUMA KASEJA

Na Mwandishi Wetu, Cairo

"NASHUKURU kwa kuniondolea adhabu niliyokuwa nimepewa, nimefarijika sana kwa hilo," hiyo ni kauli ya kipa wa Simba, Juma Kaseja.Alitoa kauli hiyo jana mjini hapa alipokuwa akizungumzia hatua ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumuondolea adhabu aliyokuwa amepewa na Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo.Kaseja alisema amepokea taarifa hizo kwa furaha kwani anaamini heshima yake kwa jamii ingeharibika na kuonekana ni kijana mkorofi wakati sivyo alivyo.Alisema tangu siku ilipotolewa adhabu alipoelezwa kuwa alikataa kupeana mkono na mgeni rasmi wa mechi ya Simba na Yanga iliyofanyika jijini Mwanza, Abbas Kandoro alipingana na jambo hilo kwani si la kiuanamichezo."Siwezi kukataa kusalimiana na Kandoro, nikaambiwa nilikataa kuwasalimia wachezaji wa Yanga, hilo pia nilienda kujitetea kwamba siwezi kufanya jambo hilo."Wengi wa wachezaji wa Yanga ni marafiki zangu, tunaheshimiana na hatuna uadui," alisema Kaseja.Wiki iliyopita Kamati ya Nidhamu ya TFF ilimuondolea adhabu ya kufungiwa mechi tatu tatu Kaseja na kulipa faini ya sh.500,000 baada ya kujiridhisha kwamba adhabu iliyokuwa imetolewa kwa kipa huyo ilikuwa na upungufu.Kamati hiyo ilieleza kuwa Kamati ya Mashindano ya TFF ilishindwa kutofautisha kati ya kukataa na kukwepa na kwamba kipa huyo alikwepa kusalimiana na wachezaji wa Yanga na hakukata, ambapo katika utetezi wake alisema hilo lilitokea baada ya yeye kushikwa na kiu na kulazimika kwenda kunywa maji wakati wenzake wakisalimiana na wachezaji wa Yanga.

Comments