BASATA YAUKARIBISHA MWAKA 2011 KWA KISHINDO

Wageni waalikwa na wafanyakazi wa BASATA wakiyarudi magoma.Hakika ilikuwa ni furaha.
Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni nchini (CAJAtz), Hassan Bumbuli akiongea jambo kwenye hafla hiyo.


Baadhi ya wafanyakazi wa BASATA wakiinamisha vichwa kwa dakika moja kwenye hafla ya kuukaribisha mwaka 2011 kama ishara ya kuwakumbuka wasanii na wadau wa sanaa waliotutoka katika kipindi cha mwaka wa 2010.


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wiki hii limefanya hafla fupi ya kuukaribisha mwaka huku Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Ghonche Materego akiwatangazia wafanyakazi kwamba,mwaka huu wa 2011 ni wa kazi na kasi kubwa katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya sanaa.
Materego alianika mikakati iliyopo kuwa ni pamoja na kuhakikisha ukumbi mkubwa wa burudani wenye uwezo wa kuchukua watu 1,000 unakamilika, tamasha kubwa la siku ya msanii wa Tanzania linafanyika kwa mafanikio makubwa, mashirikisho ya sanaa nchini yanafanya kazi kwa ufanisi na kiwango cha juu na mikakati mingine mingi.
“Mwaka huu lazima tufanye kazi kwa kasi na kiwango kikubwa,lazima ukumbi wetu wa BASATA umalizike kwa hali na mali,tamasha kubwa la msanii wa Tanzania lifanyike kwa mafanikio.Ni mwaka wa kuleta mabadiliko kwenye sekta yetu ya sanaa” alisisitiza Materego.
Aliwaasa viongozi wa mashirikisho ya sanaa nchini waliohudhuria hafla hiyo kwa niaba ya wasanii wote nchini kwamba, lazima wahakikishe wanawaunganisha wasanii katika kupigania maslahi na hki zao na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo waliyojiwekea lakini kubwa kuhakikisha mchango na takwimu sahihi za sekta ya sanaa zinapatikana.
Akiongeza zaidi alisema “Changamoto tuliyonayo mbele ni ya kuwa na takwimu sahihi katika sekta yetu ya sanaa.Kwa muda mrefu sekta yetu imekuwa ikifichwa kwenye sekta nyingine hivyo mchango wake kwenye pato la taifa kutokutambuliwa moja kwa moja.Ni wajibu wetu sasa kuhakikisha tunakuwa na takwimu sahihi za sekta hii.
Hafla hiyo fupi ya BASATA ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2011 ilifanyika kwenye viwanja vya baraza hilo na kuhudhuriwa na wafanyakazi wote,viongozi wa mashirikisho ya sanaa nchini na uongozi wa juu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Burudani.

Comments