AZAM FC YAZIDI KUTOA DOZI, YAITANDIKA AFC MABAO 5-1


TIMU ya AFC ya Arusha imeendelea kuwa ‘nyanya’ katika Ligi Kuu Tanzania bara baada ya kukubali kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Azam FC kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
AFC katika mchezo wake wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi hiyo waliocheza na Yanga walikubali kipigo cha mabao 6-1, katika dimba hilo hivyo kuwa na rekodi ya kukubali mabao 11 katika mechi mbili.

AFC ilianza kupokea kipigo cha mabao hayo katika dakika ya pili ya mchezo lililofungwa na John Bocco baada ya kazi nzuri na Ramadhani Chombo.

Baada ya bao hilo waliendelea kulisakama lango la AFC na kufanikiwa kufunga bao la pili katika dakika ya 26 lililowekwa wavuni na Ramadhani Chombo aliyeunganisha krosi safi ya Jabir Aziz.

Azam waliendelea kulisakama lango la AFC na kufanikiwa kufunga bao la tatu katika dakika ya 41 lililowekwa wavuni na Bocco aliyefanikisha kazi nzuri ya Mrisho Ngassa, mabao yalidumu hadi mwamuzi wa mchezo huo, Peter Mujaya anapuliza filimbi ya mapumziko, Azam ilikuwa mbele kwa mabao 3-0.

Kipindi cha pili Azam walirejea kwa nguvu mpya na kufanikiwa kufunga bao la nne katika dakika ya 47 lililofungwa na Mrisho Ngassa aliwahadaa mabeki wa AFC na kuukwamisha mpira wavuni.

Ngassa alifunga kalamu ya mabao baada ya kufunga bao la tano katika dakika ya 76 kwa kichwa akiunganisha kosi safi ya Peter Ssenyonjo a kuukwamisha mpira wavuni.

AFC walipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 93 lililowekwa wavuni na Jimmy Mwaisondola kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi safi ya Emmanuel Panju.

Katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Toto Africans jana iliendelea kuwa kibonde katika Ligi Kuu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1.

Mabao ya Ruvu yalifungwa na Charles Michael katika dakika ya 46 na dakika ya 72 Hassan Dilunga wakati bao la Toto lilifungwa na Hassan Said katika dakika ya 39.

Katika mchezo mwingine, Majimaji na Mtibwa Sugar jana walitoshana nguvu katika mchezo wao uliochezwa katika uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Omar Matuta katika dakika ya 32 na Ally Mohamed katika dakika ya 82 huku ya Majimaji yalifungwa na Kassim Kilugo katika dakika ya 42 na Mohamed Kijuso katika dakika ya 50.

Comments

  1. Mhhh jamani AZAM NI TIMU MOJA INAYOIBUKIA, MSIJE MKASHANGAA IKICHUKUA UBINGWA! Labda iwe nguvu ya soda

    ReplyDelete

Post a Comment