WAZIRI NCHIMBI ATAKA VAZI LA TAIFA NDANI YA MIEZI 6





Msanii maarufu wa filamu nchini James Michael (JB) akiwaeleza wajumbe wa kikao kazi cha nane cha sekta ya Utamaduni ushuhuda juu ya mafanikio yake binafsi kwenye tasnia ya filamu.Alitoa historia na changamoto zilizomkabili.
Waziri wa Habari,vijana,utamaduni na Michezo Dkt.Emmanuel John Nchimbi jana Jumanne amekifungua rasmi kikao kazi cha nane cha sekta ya utamaduni nchini kinachoendelea jijini Mwanza huku akitoa miezi sita kwa vazi la taifa kuwa limepatikana.
Pamoja na kutoa miezi hiyo sita kwa vazi la taifa kuwa limepatikana,Dkt.Nchimbi aliwahimiza watendaji wa sekta ya utamaduni kusisitiza matumizi ya sanaa za asili katika kada mbalimbali hapa nchini huku akitaka kasi iongezwe katika ukusanyaji wa takwimu mbalimbali zihusuzo wasanii na sekta ya utamaduni kwa ujumla.
“Moja ya mambo ambayo niliyaacha wakati nikiwa naibu waziri wa wizara hii ni suala la vazi la taifa,mchakato wake umekuwa ni wa muda mrefu sijui kwa nini.Sasa naagiza vazi hilo la taifa lipatikane ndani ya miezi sita kunzia sasa” alisisitiza Dkt.Nchimbi.
Aidha,aliwataka wasanii nchini kubuni sanaa zilizo bora, zenye kubeba maadili ya mtanzania na zinazoweza kuuzika kimataifa ili kuweza kujiongezea kipato.Pia alitaka elimu zaidi kutolewa kwa wasanii ili wajue umuhimu wa mikataba katika kazi zao.

Awali, akimkaribisha mheshimiwa waziri kwenye Kikao hicho,Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni,Profesa Hermans Mwansoko alisema kwamba, Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo imepata waziri kijana na sahihi ambaye atakuwa ni chachu ya mabadiliko katika sekta ya utamaduni.
Pia alimpongeza waziri aliyekuwa kwenye wizara hiyo,Mh.George Haruna Mkuchika ambaye kwa sasa amehamishiwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa utendaji wake huku akipongeza uteuzi wake kwenye wizara hiyo mpya ambapo sasa maafisa utamaduni wote watakuwa chini yake na yeye anaifahamu vema sekta hii nyeti nchini.
Akizungumzia kikao cha nane cha utamaduni kinachoendelea jijini hapa,Profesa Mwansoko alisema kwamba, kinalenga kujadili masuala mbalimbali yahususuyo sekta hii ikiwa ni pamoja na changamoto sugu zinazoikabili na baadaye kuja na njia mbadala za utatuzi.
Kikao cha sekta ya Utamaduni kinachoendelea jijini Mwanza kitafikia tamati Ijumaa ya Desemba 12, 2010 na jana wajumbe walipata wasaa wa kuelezwa hali ya tasnia ya filamu nchini ikiwa ni pamoja na kupata ushuhuda wa msanii maarufu wa filamu James Michael (JB).

Comments