TWANGA PEPETA KUTAMBULISHA ZA BOZI BOZIANA IJUMAA HII DAR WEST PARK


Na Mwandishi Wetu
Bendi ya African Stars maarufu kama Twanga Pepeta, inatarajia kutambulisha rasmi nyimbo zake mpya walizomshirikisha mwanamuziki nguli kutoka Congo Bozi Boziana siku ya mkesha wa Krismasi (Ijumaa) katika Ukumbi wa Dar West Park Tabata.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka alisema jana kuwa siku hiyo ya Ijumaa pia bendi hiyo itaonyesha video ya nyimbo hizo kwa mashabiki wake ukumbini ikiwa kama ni zawadi ya Krismasi kwa wateja wake.
Pia amesema rapa wa bendi hiyo Saul Furgasom atazindua rapi yake mpya kwenye onyesho hilo iliyoandaliwa na Bob Entertainment na kudhaminiwa na kinywaji cha Konyagi na Freditto Entertainment.
Bendi hiyo inawategemea akina Charles Baba, Dogo Rama, Msafiri Diouf, Amigolas, Saleh Kupaza, Luiza Mbutu na Janet Isinika katika safu ya uimbaji.
Kwa upande Charles Baba amesema wamejiandaa vya kutosha kuwapa burudani wakazi wa Tabata ikizingatiwa mara ya mwisho walitumbuiza kwenye ukumbi huo mwezi wa tano mwaka huu.
Naye mratibu wa onyesho hilo Joseph Kapinga amesema kuwa onyesho litakuwa la kipekee na maalum kwa kusherekea mkesha wa Krismasi .
Amesema katika onyesho hilo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa maashabiki wa bendi hiyo inayotamba na staili yake ya `kisigino.’
“Twanga Pepeta watapiga albamu zao zote. Matumaini yetu ni kuwa watu watatapata burudani ya kutosha kuliko siku zingine zote,” alisema Kapinga.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu yao yenye nyimbo tisa inayotamba kwa sasa ni Mwana Dar es Salaam ni Mwana Dar es Salaam, Shida ni Darasa, Rafiki Adui, Mwisho wa Ubaya ni Aibu, Nazi Haivunji Jiwe na Sitaku Tena.

Comments