TASWA WAIPONGEZA KILI STARS KUTWAA CHALENJI, PIA YAWAPONGEZA WANACHAMA WAKE WAMBURA, OSIAH KWA KUTWAA UTENDAJI TFF

WACHEZAJI NA VIONGOZ\I WA KILIMANJARO STARS KATIKA PIYA YA PAMOJA NA RAIS KIKWETE ALIPOWAALIKA IKULU JANA KWA CHAKULA CHA MCHANA.
RAIS KIKWETE AKIPOKEA TUZO ILIYOTOLEWA NA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO TANZANIA (TASWA), WANAOMPATIA NI MWENYEKITI WA TASWA JUMA PINTO NA MAKAMU WAKE MAULID KITENGE.

BAADHI YA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatoa pongezi kwa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kwa kutwaa ubingwa wa Chalenji mwaka 2010.
Tunaungana na Watanzania wengine katika kufurahia ubingwa huu ambao kwa miaka 16 Kilimanjaro Stars haijaupata na miaka 15 kwa Zanzibar Heroes.
Tunawaomba wachezaji watumie ubingwa wa Chalenji kama changamoto ya kufanya vizuri katika kuwania kufuzu fainali za Afrika (CAN) za mwaka 2012.
Wasibweteke na kuona tayari wamemaliza kazi, bali waendelee na jitihada za kutafuta mafanikio makubwa zaidi, huku tukiamini hakuna lisilowezekana chini ya jua.
Pia TASWA inatoa pongezi kwa Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah na Ofisa Habari wa shirikisho hilo Boniface Wambura kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.
Osiah na Wambura ni wanahabari wazoefu, ambao kwa muda mrefu wamepata kuwa wahariri wa habari za michezo na ni watu wenye kujua mambo mengi yanayohusu kazi zao mpya.
Lakini pia Wambura amekuwa Mwenyekiti wa TASWA kwa miaka sita mfulululizo, pia amepata kukaimu nafasi hiyo ya uenyekiti kwa miaka miwili, ni mtu mzoefu kwenye mambo ya habari hasa yanayohusiana na usimamizi wa wanahabari.
Tunaamini watakuwa watendaji wazuri kwa nafasi hiyo na kama ni pumu basi tunasema zimepata mkohozi, TASWA inaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.
Tunawatakia kila la heri Osiah na Wambura huku tukiamini hawatawaangusha Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF w waliowaamini kushika nafasi hizo.
Lakini tunawapa changamoto waelewe kuwa kutekeleza na kutelekeza ni maneno ni maneno mawili yanayoshabihiana katika kuyatamka na usipokuwa makini yanaweza kukuchanganya na kukupoteza kabisa.
Lakini haya ni maneno yenye maana tofauti, ambazo moja ni kama chanya na nyingine hasi. Neno kutekeleza maana yake kwa tafsiri rahisi ni kufanya, wakati kutelekeza maana yake ni kutofanya, kuacha au kupuuzia.
Tunawaombea heri watekeleze majukumu yao kwa ufasaha na wala si vinginevyo, huku tukiwaambia Osiah na Wambura wakumbuke kwamba gari ya makanika hailali njiani.
Wao ni kama fundi makanika, tutashangaa sana kama gari ikiharibika halafu wao wamo ndani kisha wakakubali kulala porini.

Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
14/12/2010

Comments