NEW HABARI 2006 YAIPIGA JEKI TIMU YA NETIBOLI KINONDONI

OFISA MKUU MTENDAJI WA NEW HABARI 2006, HUSSEIN BASHE AKISALIMIANA NA WACHEZAJI WA TIMU YA NETIBOLI YA KINONDONI
KAMPUNI ya New Habari 2006, Mbunge wa Kinondoni Idd Azan na Mbunge wa Ubungo John Mnyika, wameipiga jeki timu ya netiboli ya Manispaa ya Kinondoni inayoshiriki michuano ya Kombe la Taifa iliyofunguliwa jana kwenye viwanja vya Shule ya Filbert Bayi iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Awali, timu hiyo ilikuwa katika hatihati ya kushiriki mashindano hayo kutokana na kukabiliwa na ukata, lakini hatimaye iliondoka jijini Dar es Salaam jana jioni baada ya kuwezeshwa na wabunge hao na New Habari ambao ni watengenezaji wa magazeti ya Bingwa, Dimba, Mtanzania, Rai na The African.
Wakati Azan akitao usafiri na kugharamia mahitaji mengine ya timu hiyo, New Habari na Mnyika walichangia fedha taslimu kwa ajili ya kusaidia posho na matumizi mengine ya wachezaji wa timu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Msaidizi wa Chama cha Netiboli Manispaa ya Kinondoni (CHANEKI), Michael Maurus, alisema kuwa baada ya kuona hali ni tete juu ya ushiriki wa timu hiyo katika mashindano hayo, waliamua kuomba msaada kutoka kwa watu mbalimbali na kufanikiwa katika hilo.
“Tunamshukuru Azan kwa sapoti yake, pamoja na Mnyika ambaye tulimfahamisha tatizo hilo leo (jana) na akakubali wakati huo huo kutusaidia kama ilivyokuwa kwa uongozi wa New Habari chini ya Ofisa Mkuu Mtendaji wake, Hussein Bashe aliyejulishwa tatizo hilo wakati timu hiyo ikiondoka,” alisema Maurus ambaye ni mfanyakazi wa New Habari.
Maurus aliwataka wadau wa michezo wa Kinondoni kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali kwani itakapokuwa katika michuano hiyo, inahitajika kujigharamia kwa chakula ambacho ni Sh 5,000 kwa kila mchezaji kwa siku, pamoja na posho za wachezaji na maji.

Comments