MAAZIMIO 16 YAPITISHWA KATIKA KIKAO CHA UTAMADUNI, CHAMALIZIKA RASMI HII LEO

Mgeni rasmi kikao kazi mkuu wa mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro, akikiahirisha rasmi kikao cha nane cha sekta ya utamaduni kwa mwaka wa 2010.
Kikundi cha ngoma za asili cha Chapakazi kikicheza Ngoma ya Bugobogobo mbele ya wajumbe wa Kikaokazi cha nane cha Sekta ya Utamaduni.Ngoma hii ni maarufu kwa wenyeji wa Mkoa wa Mwanza ambao ni Wasukuma.

Na Mwandishi Wetu,Mwanza
Kikaokazi cha nane cha sekta ya utamaduni kilichokuwa kikifanyika jijini Mwanza kwenye ukumbi wa BoT na kubeba kaulimbiu ya Sanaa ni ajira tuithamini kimefikia tamati huku kikipitisha maazimio 16 ya kufanyiwa kazi na wadau mbalimbali.
Akiongea wakati wa kufunga kikaokazi hicho,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kwamba,sekta ya utamaduni hususan sanaa ni muhimu haipaswi kudharauliwa bali ya kupewa kipaumbele,kuthaminiwa na kutumika kama alama ya kulitambulisha taifa letu kote duniani.
“Watu wanadhani sanaa ni ya mchezo tu,sanaa ni utambulisho mkubwa sana kwa taifa letu.Nashukuru kwa kaulimbiu ya mwaka huu ya kikao hiki kwamba sanaa ni ajira tuithamini,naamini vipaji tunavyo vingi hapa nchini ni lazima tujitume, tuvitafute na tuviendeleze” alisisitiza Kandoro.
Aliongeza kwamba,sanaa zinazotengenezwa na wasanii wetu lazima ziwe na ubora mkubwa ili ziwape faida, zisiwe za kuiga, ziwe zenye maadili ndani yake zaidi zibebe kweli kaulimbiu ya sanaa ni ajira.Aidha,alihimiza ubunifu miongoni mwa wasanii ili wananchi nao wavutiwe kuzipenda na kuzithamini.
“Huwa nachukizwa sana na maadili katika sekta ya sanaa.Hivi kuna ulazima gani wa wasanii kuvaa uchi na kujidhalilisha kwa mambo ya kuamsha hisia za ngono majukwaani na kwenye video? Sanaa inatakiwa itumike katika kujenga uzalendo na maadili miongoni mwa wanajamii kama kupambana na VVU/UKIMWI lakini kwa sasa inaonekana kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili na kusababishwa kusambaza virusi” aliongeza Kandoro.
Kuhusu kikaokazi hicho Kandoro alisema kwamba, ni vema maazimio mbalimbali yaliyofikiwa yakafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuingizwa kwenye bajeti za wilaya, zile za taaisisi za umma na na za wizara vinginevyo yatabaki kuwa kwenye makabrasha bila kufanyiwa kazi yoyote.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi,Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Sethi Kamuhanda alisema kwamba,wadau mbalimbali wa sekta ya utamaduni wamekuwa kwa wiki nzima wakiijadili sekta hiyo na hivyo kazi kubwa iliyoko mbele ni kutekeleza maazimio yote yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kuyaweka kwenye bajeti na mipango mikakati.
Kikaokazi cha nane cha sekta ya utamaduni kilichokuwa kikifanyika jijini Mwanza kwenye Ukumbi wa BoT kilinza Desemba 13 na kufikia tamati Desemba 17,2010.Kimetoka na maazimio 16 ambayo yanapaswa yafanyiwe kazi katika kipindi cha mwaka mmoja.

Comments