BASATA YAWAPA SEMINA ELEKEZI MAJEMBE KUMULIKA KUMBI ZISIZOSAJILIWA



Baada ya mapema wiki hii Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kutiliana saini na Kampuni ya Udalali ya Majembe kufuatilia kumbi za Sanaa na Burudani zisizosajiliwa na kufuata sheria na kanuni zilizopo, leo Ijumaa Baraza limeanza rasmi kuwapa semina watendaji wa kampuni hiyo ili kuendesha zoezi hilo kwa ufanisi na kwa uamkini. Semina hiyo ya siku moja inayojikita kwenye kufafanua majukumu ya Baraza, aina ya kumbi na sifa zake, wadau wanaopaswa kusajiliwa,umuhimu wa usajili na mipaka ya utendaji ya kampuni hiyo imeendeshwa na watendaji wa BASATA kupitia kamati yake ya usajili na vibali chini ya Mwenyekiti A.G.M Luhala inatazamiwa kuwapa watendaji hao wa Majembe uzoefu na dira ya kutekeleza zoezi zima la urasimishaji wa kumbi na baadaye tasnia ya sanaa kwa ujumla. Akizungumza kwenye semina hiyo,Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya BASATA,Bw.Luhala alisema kwamba,kwa mujibu wa sheria ya Bunge Na.23 ya mwaka 1984,Baraza limepewa mamlaka kusajili chama, asasi, kumbi, wasanii na wadau wote wanaojihusisha na shughuli za sanaa na kwamba kufanya vinginevyo ni kuvunja sheria za nchi. “Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 kifungu cha 4 (1) (h), 15 (d-e),na kanuni za BASATA tangazo la Serikali namba 322 la tarehe 21/10/2005), Baraza limepewa mamlaka kisheria ya kufanya usajili wa watu,vikundi,asasi,vyama na kumbi zinazotumika kwa maonyesho ya sanaa na burudani.Kufanya bila kufuata sheria na kanuni hizi ni kukiuaka sheria za nchi. Sheria ndogo za BASATA namba 322 za mwaka 2005 kifungu cha 17 (1-28) zinazumgumzia haja ya wadau wote wa sekta ya sanaa kujisajili na kulipia vibali vyao kwenye Baraza.Mfano kifungu kidogo cha 2 kinasema,hakuna chama au asasi itakayoruhusiwa kuendesha shughuli za sanaa bila kusajiliwa” alisisitiza Luhala. Awali akifungua semina hiyo,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,zoezi la usajili wa kumbi ni sehemu ya kuwataka wamilki wake kufuata sheria, kanuni na taratibu pia kutekeleza tamko la Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Bw.Sethi Kamuhanda la Septemba 20/2010 lililowataka wamiliki wote wa kumbi kuzisajili kabla ya Desemba 31/2010.

Comments