BASATA YAJA NA MAPINDUZI KATIKA SEKTA YA SANAA NCHINI

Dkt.Amos Mwakilasa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Utamaduni na Mjumbe wa Kamati ya Maudhui ya TCRA naye alichangia kwenye Mpango mkakati huo wa BASATA.Aliupongeza lakini akataka msisitizo uwekwe kwenye kufundisha stadi za sanaa toka ngazi ya shuke za awali.


Na Mwandishi Wetu,Mwanza
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza kuja na mikakati mizito ya kukuza sekta ya sanaa nchini ikiwemo kujenga jumba kubwa la sanaa ambalo litakuwa na hosteli za wasanii kwa ajili ya wao kuishi wakati wakiandaa kazi zao mbalimbali za sanaa.
Akiwasilisha mpango mkakati wa maendeleo wa BASATA kwa mwaka 2011-2014 kwenye Kikao cha nane cha utamaduni kinachofikia tamati wiki hii jijini Mwanza,Katibu Mtendaji wa baraza hilo,Ghonche Materego alisema kwamba lengo la nyumba hiyo ya sanaa ni kuandaa eneo maaulum kwa ajili ya wasanii kuandalia kazi zao na kufanya maonyesho mbalimbali.
Mbali na jumba hilo la Sanaa,Materego alisema kwamba,BASATA iko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha ukumbi mkubwa wa sanaa na burudani wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 1,000 wakiwa wamekaa ambao unatazamiwa kufufua rasmi sanaa za maonyesho ya jukwaani ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na kukosekana kwa eneo maalum la kuzionyesha na kuziuza.
“Ndugu wajumbe, ni matarajio ya Baraza kwamba, nyumba na ukumbi huu wa sanaa na burudani ulio katika hatua za mwisho vitakapokamilika kutakuwa na uhai mkubwa wa sekta hii hapa nchini kiasi cha kuanza kukita mizizi kwa watanzania wengi hususan wale wasiyothamini sanaa za nyumbani” alisisitiza Materego.
Akizungumzia suala la haki na wizi wa kazi za wasanii,Materego alisema kwamba, pamoja na kuwepo mamlaka nyingine inayoliangaza,Baraza katika mpango mkakati wake linakusudia kuunda kitengo maalum cha kulifuatilia hasa kwenye sanaa za asili ili kuhakikisha linapungua ili kuimarisha kipato cha wasanii.
Aidha,Materego alisema kwamba muda umefika sasa wa kuwepo kwa sera ya sanaa inayojitegemea badala ya ilivyo sasa ambapo,sekta hiyo ambayo inakua kwa kasi na kuwa tegemeo la vijana wengi imebebwa ndani ya ile ya utamaduni inayobeba mambo mengi sana.
“Baraza linakusudia kushawishi kupitia njia mbalilmbali ili sera ya taifa ya sanaa iundwe na baadaye kuleta mageuzi makubwa katika tasnia hii.Hakuna sababu ya sekta ya sanaa kufichwa ndani ya sera ya utamaduni kwani kwa sasa imekua sana na kuhitaji muongozo huru wenye kuhitaji uratibu wa kitaifa wa moja kwa moja” aliweka msisitizo Materego.
Alisema kwamba, pamoja na sekta ya sanaa kuongozwa na sera ya utamaduni ya mwaka 1997 bado sheria za Baraza ile ya Bunge na zile ndogonmdogo zinazosimamia sekta hii ni za mwaka 1984 hali inayohitaji kufanyiwa marekebisho makubwa.
“Ndugu wajumbe, sheria zilizounda Baraza za mwaka 1984 ni za muda mrefu sana kwa sasa Baraza katika mpango mkakati wake huu linalenga kuzifanyia marekebisho makubwa ili kukidhi muda na matakwa mbalimbali kwa ajili ya usimamizi na uendelezaji wa sekta ya sanaa” alimalizia Materego.
Baraza la Sanaa la Taifa ni shirika la umma lililoundwa kwa sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 na kazi zake kubwa ni kuratibu matukio ya sanaa nchini, kusimamia na kukuza sekta ya sanaa nchini kupitia kuhimiza ubunifu wa sanaa bora.

Comments