BASATA YAINGIA MKATABA NA MAJEMBE KUDHIBITI KUMBI NA WADAU WA SANAA WASIYOSAJILIWA NA KUFUATA SHERIA

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wiki hii limeingia rasmi mkataba na kampuni ya ukusanyaji madeni na udalali ya Majembe kwa ajili ya kudhibiti kumbi ambazo hazijasajiliwa na zinazofanya kazi kinyume cha sheria,kanuni na taratibu zilizopo.
Mkataba huo ambao kwa kuanzia utafuatilia kumbi zote za sanaa na burudani nchini kabla ya muda mfupi ujao kugusa wadau wote wa tasnia hii wakiwemo wasanii unalenga kuleta urasmi wa sekta na kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zote zinafuatwa ili kuepuka maafa na matatizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakijitokeza na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba,Baraza liko kwenye mkakati kabambe wa kuirasimisha sekta ya sanaa na burudani na kwa kuanzia wamiliki wote wa kumbi lazima wahakikishe wamezisajili kumbi zao na kuhakikisha zinakidhi matakwa kufuatana na sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji.
Aliongeza kwamba,BASATA imekuwa ikiwakumbusha wamiliki wa kumbi na wadau wote wa sanaa juu ya haja ya kufuata sheria, kanuni na taratibu lakini muitikio umekuwa mdogo hivyo kwa sasa Baraza limeona ni vema kuwapa kazi Majembe ili kuhakikisha kumbi zote nchini zinakidhi matakwa yaliyopo na kuepuka mianya ya maafa kutokea.
“Muda umefika sasa wa sekta ya sanaa na burudani kuwa rasmi,ninawaomba wamiliki wa kumbi waoneshe ushirikiano mkubwa katika hili lakini pia wadau wote wa tasnia hii nao wahakikishe wanajisajili na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi” alisisitiza Materego.
Akizungumza baada ya zoezi la utiliaji saini,Mkurugenzi wa Kampuni ya Majembe,Seth Motto alisema kwamba,vijana wake wako tayari kwa kazi hiyo na wamejipanga kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Aliongeza kwamba,kampuni yake imekuwa ikifanya oparesheni nyingi hapa nchini kwa mafanikio makubwa hivyo ni lazima wamiliki wa kumbi za sanaa na burudani na wadau wote wa tasnia hii kuonesha ushirikiano wa dhati na kuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo mbalimbali watakayokuwa wakipewa.

Comments