VODACOM TANZANIA YAKABIDHI MAGARI 100 KWA WASHINDI WA PROMOSHENI YA SHINDA MKOKO

Maijo Hamisi akishangilia baada ya kukabidhiwa gari lake alilojishindia katika promosheni ya shinda mkoko ambapo jumla ya washindi 100 walikabidhiwa magari yao,Kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Dietlof Mare.

Mkurugenzi wa mahusiano wa Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Dietlof Mare wakifuatilia hafla ya kukabidhi magari 100 aina ya Hyundai i10 yaliyotolewa na kampuni hiyo kwa washindi wa shindano la shinda mkoko . 

KAMPUNI ya simu ya mkononi ya Vodacom Tanzania kupitia promosheni yake ya 'Shinda Mkoko' (leo) imekabidhi magari 100 aina ya Hyundai i10 kwa washindi wake ikiwa ni ishara ya kukamilika kwa shindano hilo lilianza rasmi Agosti 2 mwaka huu.

Katika promosheni hii iliyochukua takribani siku 100 kila siku mteja mmoja wa Vodacom Tanzania alizawadiwa gari ambapo hadi bahati nasibu hii inafikia mwisho wake ikiwa ni maadhimisho ya miaka kumi ya utoaji huduma wa kampuni hiyo nchini tayari jumla ya washindi 100 walikwishapatikana.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Dietlof Mare alisema kwa kutambua umuhimu wa jamii inayofanya nayo biashara kampuni yake iliona irudishe kiasi cha faida wanayoipata kwa wananchi ili kiwasaidie.
"Katika kusherehekea maadhimisho haya ya utoaji huduma zenye mafanikio kwa wateja wetu na jamii kwa ujumla, tumeona tutumie fursa hii ya kumbukumbu ya miaka kumi ya utendaji wa Vodacom Tanzania kwa kurudisha faida iliyopatikana kwa wateja wetu," alisema Mare.
Akifafanua alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya utoaji huduma nchini Vodacom imejiwekea utaratibu wa kutoa huduma bora tena za kipekee na uanzishwaji wa promosheni mbalimbali kwa lengo la kuiwezesha na kuinua kichumi jamii ya Watanzania.
"Licha ya kuwazawadia magari 100 wateja wetu mbalimbali, pia mtandao wetu una wateja takribani milioni 6 waliojiunga kwenye huduma ya kutuma na kupokea fedha ya M-Pesa iliyoenea kote nchini," alisema.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo Ephraim Mafuru alisema shindano hilo liliwahusisha wateja wote wa kampuni hiyo nchini waliofika kutoka maeneo tofauti nchini kupokea magari yao.
Aidha aliongeza kwamba washindi katika promosheni hiyo walipatikana baada ya kuwa na pointi nyingi walizojikusanyia ambazo zilichezeshwa kwenye droo ili kumpata mshindi wa promosheni hiyo kila ilipochezeshwa.
"Wakati promosheni inaendelea baadhi ya watu walidai tusingeweza kugawa magari haya 100 kwa kuwa ni wababaishaji, lakini kupitia bodi ya michezo ya kubahatisha nchini (TGB) leo tumetimiza lengo letu na kuwazawadia washindi magari yao," alisema Mafuru.
Kwa upande wake Meneja Mtendaji wa New Dodoma Hoteli Wellingtone Maleya alisema hafla hiyo imeondoa dhana kwamba wateja walikuwa wanapeleka fedha Vodacom ili watangazwe washindi hali ambayo imedhihirika kwamba ni uzushi.
"Leo tunashuhudia wateja wa matabaka tofauti wakikabidhiwa magari yao, wengine ni mameneja, akina mama wa nyumbani na hata shamba boy. Kama ingekuwa kupeleka hela Vodacom ndio kushinda leo tungekutana tunaojiweza watupu hapa," alisema Maleya.
Hyundai i10 ni gari inayohimili mazingira ya mijini (hatchback) ambayo imetengenezwa na Kampuni ya magari na mitambo ya Hyundai Motor Company, na lilizinduliwa rasmi nchini Oktoba 31, mwaka 2007.
Gari hiyo ya gharama nafuu ni rahisi kuihudumia kwani inatumia kiwango kidogo cha mafuta ikiwa pia tofauti na magari mengine ambayo unapoyatumia unajisikia raha na kukuweka huru.

Comments