TASWA YAIPONGEZA TIMU YA TAIFA YA GOFU YA WANAWAKE

KATIBU MKUU WA TASWA, AMIR MHANDO
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinatoa pongezi kwa timu ya Taifa ya gofu ya wanawake ya Tanzania ambayo mwishoni mwa wiki iliweka historia katika michuano ya gofu ya Wanawake ya Kombe la Challenge Afrika, baada ya kushika nafasi ya pili kwenye michuano iliyofanyika viwanja vya Klabu ya IBB International mjini Abuja.

Tanzania ilishika nafasi ya pili kati ya nchi 14 za Afrika baada ya kukusanya jumla ya mikwaju 474 katika raundi tatu za viwanja vya IBB vyenye par 74, ambapo Afrika Kusini iliyokuwa ikitetea taji hilo iliibuka tena bingwa kwa kukusanya mikwaju 440.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Zimbabwe iliyokuwa na mikwaju 475, huku Zambia wakishika nafasi ya nne mikwaju 485.
Tunawapongeza wachezaji wa timu hiyo, viongozi na wadau wengine wote waliofanikisha safari ya timu hadi kufanikisha ushindi huo, kwani hiyo ni mara ya kwanza kwa gofu wanawake kupata matokeo mazuri kama haya, hasa tukikumbuka kuwa michuano kama hiyo iliyofanyika Cairo, Misri mwaka 2008 Tanzania ilishika nafasi ya 8.
Taswa imefurahishwa na matokeo hayo, kwani yamekuja wiki chache baada ya timu hiyo kushindwa kung’ara katika michuano ya Dunia iliyofanyika Buenos Aires, Argentina.
Lakini pia yametufariji zadi hasa baada ya wanamichezo wa Tanzania kushindwa kung’ara katika michuano ya Nchi za Jumuiya ya Madola iliyofanyika India miezi michache iliyopita.
Tunawaomba wachezaji wa gofu waliokuwa Abuja, Nigeria, Hawa Wanyeche, Madina Iddi na Shazi Myombe wasibweteke na mafanikio hayo bali waongeze juhudi zaidi wazidi kuitangaza nchi.
Tunatoa wito kwa wadau waangalie na michezo mingine na kuiunga mkono na wasiegemee aina fulani ya michezo, hata kama haifanyi vizuri. Hili wenzetu wa gofu wamelithibitisha vizuri.

Ahsante,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA

Comments