NIMEKUJA KUIFUNGIA MABAO YANGA- MWAPE

MSHAMBULIAJI wa kimataifa kutoka Zambia, Davies Musonda Mwape amesema amekuja kujiunga na Yanga kwa kazi moja tu ya kuifungia mabao ili kuipatia mafanikio katika mechi za kitaifa na kimataifa.

Davies aliyetua nchini Jumatatu mchana kwa ajili ya majribio katika timu ya Yanga waliopo kwenye mkakati wa kupigania ubingwa wa 22 tangu 1965, alisema kama atasajiliwa, atajitahidi kufunga mabao kwani ndiyo kazi iliyomleta Tanzania.
Mwape aliyetua Yanga akitokea klabu ya Kankolo Blades ya Ligi Kuu nchini Zambia, alisema kama mipango yake itakwenda vizuri, ataanza kuichezea timu hiyo kwenye raundi ya pili ya Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.
Akizungumza  jijini Dar es Salaam, nyota huyo aliyewahi kukipiga Orlando Pirates na Jomo Cosmos za Afrika Kusini, alisema kitu muhimu ni kwenda kwa mazungumzo na kupewa ushirikiano na wenzake dimbani.
Alisema kama mipango ya kuichezea Yanga itafanikiwa, atajitahidi kadiri ya uwezo wake kushirikiana na wachezaji wenzake kuipatia timu hiyo mafanikio kwani ndiyo zawadi pekee anayoweza kuwapa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
“Nimekuja kufanya majaribio ya kuichezea Yanga…bado sijafanikiwa lengo hilo kwani sijasaini mkataba, lakini mambo yanakwenda vizuri, nikifanikiwa, nitajitahidi kuipatia mafanikio kwa kuifungia mabao mengi kwani hiyo ndiyo kazi niliyoifuata,” alisema kwa kujiamini.
Alisema ingawa haifahamu sana Yanga na soka ya Tanzania kwa ujumla, lakini anaamini ni timu bora na yenye malengo, hivyo kwa kipindi ambacho atakuwa katika timu hiyo, atajitahidi kuzoea mazingira na kutimiza wajibu wake dimbani.
“Sijawahi kufika Tanzania na wala siifahamu vizuri Yanga na hakuna mchezaji ninayemfahamu Yanga na Tanzania, …lakini kubwa ni kuhakikisha natimiza majukumu yangu dimbani, hicho ndicho kikbwa,” alisema nyota huyo mrefu na umbile lililojaa.
Mwape aliongeza kuwa, kuja kwake Tanzania, kunatokana na kufahamiana vizuri na kocha wa Yanga, Kostadin Papic aliyeanza kuinoa Yanga Oktoba mwaka jana akichukua nafasi ya Dusan Kondic.
Yanga na timu nyingine za Ligi Kuu, zipo katika harakati za usajili mdogo utakaofikia tamati Novemba 30; kwa lengo la kuviongezea nguvu vikosi kuelekea raundi ya pili ya ligi hiyo itakayoanza Januari, mwakani
Hadi raundi ya kwanza inafikia tamati Novemba 7, Yanga inakamata nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 25 huku mtani wake Simba, bingwa mtetezi wa ligi hiyo, akiongoza kwa pointi 27.

Comments