MASHIRIKISHO YA SANAA YAJA NA MIKAKATI MIZITO YA KUWAKOMBOA WASANII

1. Rais wa Shirikisho la Filamu, Symon Mwakifwamba (Kulia) akionesha moja ya habari kwenye gazeti iliyokuwa na taarifa za uvunjifu wa maadili za mmoja wa wasanii wa filamu.Aliahidi kupambana na hali hiyo katika tasnia ya filamu.

Mashirikisho ya Sanaa nchini yametaja mikakati ya kuikomboa tasnia ya sanaa dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mipango madhubuti inawekwa katika kuwafanya wasanii kuwa na maisha bora na kufanya kazi zenye ubora na zinazokubalika ndani na nje ya nchi.
Marais wa mashirikisho hayo ambao ni Symon Mwakifwamba (Filamu), Adrian Nyangamale (Ufundi), Ibra Washokera (Muziki) na Agnes Lukanga (Maonyesho) waliweka wazi mikakati hiyo wakati wakiwasilisha mada kwa pamoja (Panel Discussion) kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii katika Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Baadhi ya mikakati iliyotajwa na marais hao ni ya kuhakikisha sheria ya hakimiliki na haki shiriki inaangaliwa upya, kupambana na maharamia wa kazi za wasanii, kujenga mtandao mpana wa mashirikiano baina ya wasanii,kuimarisha uongozi wa vyama mbalimbali vya wasanii, kupambana na unyonyaji dhidi ya wasanii na kujenga maktaba za sanaa (Art Galleries) ambamo kazi mbali za sanaa zitahifadhiwa.
Rais wa Shirikisho la Filamu Symon Mwakifwamba yeye aliweka wazi kwamba, kazi kubwa waliyonayo ni kupambana na maharamia wa kazi zao, kuandaa tuzo za filamu (people’s choice awards) ambazo zinatazamiwa kufanyika Februari mwakani, uvunjifu wa maadili na tabia chafu za wasanii wa filamu ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikilalamikiwa na wadau kiasi cha kuacha maswali mengi juu ya hatma ya wasanii wa tasnia hiyo.
Tuna mikakati mizito ya kupambana na maadili machafu katika filamu, tabia za kukaa nusu uchi, kufanya mambo ya aibu haivumiliki, sisi tunajipanga kuweka kanuni za adhabu ambazo zitadhibiti maadili katika filamu na wasanii wake.Hili tutalisimamia kwa kuweka adhabu za vifungo vya muda mfupi na mrefu kwa wasanii ili wasishiriki katika kucheza filamu” aliongea kwa hasira Mwakifwamba huku akionesha moja ya gazeti lililokuwa na habari chafu za mmoja wa wasanii wa filamu.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi,Bw.Nyangamale alisema kwamba,shirikisho lake linajipanga kujenga maktaba kubwa ya sanaa (Art Gallery) ambayo ndani yake kutawekwa kazi za sanaa za ufundi kama vinyago, nguo zilizobuniwa na wasanii wa ndani, michoro nk.Aidha, aliongeza kwamba, wanajipanga kuzindua rasmi shirikisho,kufanya utafiti juu ya sanaa mbalimbali za ufundi zinazopatikana nchini na mikakati mingine mingi.
Nalo shirikisho la muziki kupitia Rais wake Ibra Washokera liliweka wazi kusudio la kuwabana watumiaji wa muziki hasa wamiliki wa Madisko,Radio na TV ili kuwalipa wasanii mirahaba,kukusanya kazi za muziki za zamani na mpya,kukusanya taarifa za wasanii wa muziki, kutanua mtandao wa shirikisho na kuandaa kongamano kubwa la muziki nchini.
Wadau wengi walipongeza juhudi za mashirikisho haya lakini wakashauri kuwe na mikakati ya muda mfupi na mrefu katika kuyafikia malengo hayo.

Comments

  1. Ndugu Mwakifwamba nakupongeza sana kwa initiative hiyo maana kweli wasanii wengi wanaichafua tasnia hiyo. Mfano mzuri ni huyo mtoto Lulu (Elizabeth)kwa kweli anatia kinyaa, mtoto mdogo kama yeye kufanya mambo ya kikahaba kama hayo utadhani hana wazazi, inasikitisha. At her age hakutakiwa kwenda ktk kitchen party, nashangaa nini kilimpeleka huko (ktk kichn party ya Thea). Anafanya hata sisi wazazi ambao tuna watoto wana vipaji tuogope kuwaruhusu kuingia katika tasnia hiyo sababu ya kuhofia na wao kubadilika kuwa na tabia chafu. Huyo mtoto ana tabia chafu na ikiwezekana asipojirekebisha afungiwe kufanya kazi hiyo. Mimi ni mzazi mwenye uchungu............ KIUKWELI NIKIMUONA HUYO MTOTO HUWA NATOKWA NA GOOSE BUMPS (VIPELE) MWILINI KWA SABABU YA TABIA YAKE CHAAAFU!!!!

    ReplyDelete

Post a Comment