MALARIA HAIKUBALIKI NA CECAFA TUSKER CUP 2010

Leo tarehe 26 Novemba 2010 hapa Dar es Salaam, katika mkutano wa waandishi wa habari kufungua mashindano ya Tusker Challenge yanayo anza kesho, washiriki na wadau wa kampeni ya “Tuungane Kutokomeza Malaria” - United Against Malaria (UAM) wameungana na wandaaji wa mashindano kumulika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Eneo hili la Afrika watu wapatao Milioni 38.9 huugua Malaria miongoni mwao wakiwa watoto.

Zaidi ya watu 209,000 hufariki kila mwaka ikiwa ni karibu robo ya vifo vyote vya malaria vinavyotokea barani Afrika. Malaria ni ugonjwa unao zuilika na kutibika ilihali kila sekunde 45 mtoto mmoja hufariki kwa Malaria na kusababisha hadithi za huzuni na umasikini.
Rais wa shirikisho la mpira la CECAFA Ndugu Leodegar Tenga alisema,” Mchezo wa mpira wa miguu unataka jamii yenye afya ili uendelee na kukua. Wanahitajika makocha, wachezaji, wasimamizi, marefa na hasa mashabiki wenye afya. Bila watu wenye afya hatuwezi kuendeleza soka. Jamii yenye Malaria haina afya, ndio maana tunaunga mkono juhudi za kutokomeza malaria zinazofanywa na kampeni ya United Against Malaria”
Timu 12 za Afrika Mashariki na Kati pamoja na washiriki wageni kutoka Malawi, Zambia na Ivory Coast zimekusanyika hapa Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano ya CECAFA, uongozi wa juu wa CECAFA umetangaza kushiriki kikamilifu katika kampeni za kutokomeza Malaria na kuhakikisha wanatumia mbinu zote za kuzuia wachezaji kupata Malaria ikiwa ni ahadi yake ya kujiunga na kampeni ya UAM.
“UAM imepata ushirikiano wa hali ya juu kutoka CECAFA, hii inadhihirisha dhamira yao ya kushiriki katika vita dhidi ya Malaria.” kasema David Kyne, Meneja wa kampeni ya UAM. Mashirikisho ya soka, timu za mataifa na wachezaji watatumia umaarufu wao katika michezo kuelimisha jamii zao dhidi ya umuhimu wa matumizi ya njia zote zinazoshauriwa na wataalamu za kujikinga au kutibu Malaria kama vile vyandarua, kupima na kutumia dawa endapo wataambukizwa malaria.
Ili kuthibitisha jitihada za sekta binafsi kuunga mkono kampeni ya UAM, mdhamini wa mashindano ya CECAFA atashawishi makampuni mengine yajiunge na kampeni na kusisitiza umuhimu wa wafanyakazi na wateja wao kuwa salama kwa kutumia kinga ama tiba dhidi ya Malaria.
“Kama wadhamini wa CECAFA Tusker Challenge Cup 2010 tunaungana na kampeni ya United Against Malaria kwa kuhakikisha wafanyakazi wetu wanapata kinga na tiba dhidi ya Malaria kwa muda wote.” Alisema Caroline Ndugu, Mkurugenzi wa Masoko wa Serengeti Breweries Limited. Aliongeza ”Leo hii tuna ahidi kununua vyandarua vyenye dawa ya kuzuia mbu wa Malaria kwa wafanyakazi wetu wote hapa Tanzania”
Njia mbalimbali za kufikisha ujumbe wa malaria kwa jamii ambazo zitatumika muda wote wa mashindano ni pamoja na matangazo yatakayorusha katika vyombo vya habari kama redio, runinga na mtandao wa internet, mabango yenye ujumbe wakati wa kila mechi na nguo za mazoezi ya awali kwa timu kabla ya mechi pamoja na ujumbe kwenye programu ya mashindano.

Comments