ABDI KASSIM ANA THAMANI YA SH.MILIONI 100

YANGA imesema thamani halisi ya nyota wake Abdi Kassim ‘Babi’, ni shilingi mil.100, hivyo timu itakayomtaka, italazimika kutoa kiasi hicho kumpata nyota huyo aliyepo nchini Vietnam akifanya majaribio katika klabu ya Dong Tam Long An.

Mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga alisema jana, huo ni uamuzi wa uongozi kama atafuzu majaribio hayo watamuuza kwa kiasi hicho cha fedha na si kinyume na hapo.
“Uongozi umeamua kuwa kama klabu hiyo ana yoyote itakayotaka kumnunua haina budi kulipa kiasi hicho cha fedha, kinyume na hapo suala lake la kuuzwa lifungwe hadi mwishoni mwa msimu wa 2010/2011,” alisema Nchunga ambaye ni mwanasheria kitaaluma.
Nchunga alisema, Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti wa kamati ya mashindano kuendelea kuhangaikia Uhamisho wa Kimataifa (ITC) cha Kenneth Assamoh kumwezesha kucheza ngwe ya pili ya Ligi Kuu itakayoanza Januari 15, mwakani.
“TFF kupitia raisi wake Tenga (Leodegar), imekuwa na mawasiliano na FIFA kuhusiana na suala hili, pia tumemuagiza kocha wetu Papic (Kostadin) kupitia Zurich (Makao makuu ya Fifa) kufuatilia kwa ukaribu suala hili,” alisema Nchunga.
Katika hatua nyingine, uongozi umeamua kuliweka kando suala la kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani Mrisho Ngassa kutoka Azam mpaka hapo itakapoamriwa baadaye.
Aidha, katika kuiamarisha kikosi cha timu hiyo, wapo mbioni kumsajili mshambuliaji kutoka Visiwani Zanzibar, Ally Shiboli na viungo wengine wawili wasio wa ikimataifa.
Katika hatua nyingine, mfadhili wa klabu hiyo Yusuf Manji amejitolea kulipa gharama ya dola 3,000 za Marekani za matibabu kwa mchezaji atakayepata matatizo na kushindwa kutibiwa nna kituo cha Trauma Center kwa sababu kadha wa kadha.

Comments