TIP TOP CONNECTION YAMBEMBA MSANII TOKA THT

MSANII TOKA THT 'KWEA PIPA'
MENEJA wa kundi la muziki wa kizazi kipya nchini la Tip Top Connection Babu Tale ametoa ofa ya kumpeleka studio msanii kutoka Tanzania House of Talent (THT), anayejulikana kwa jina la ‘Kwea Pipa’.

Meneja huyo, amefikia uamuzi huo baada ya kuvutiwa na kipaji cha hali ya juu alichokionyesha msanii huyo siku ya mahafali ya wanafunzi wa THT yaliyofanyika hivi karibuni kituoni hapo, Kinondoni Block 41 jijini Dar es Salaam.
Katika mahafali hayo, Kwea Pipa ambaye alikuwa ni mmoja wa wahitimu, aliweza kukonga nyoyo za waliohudhuria kupitia kibao chake kinachokwenda kwa jina la ‘Sasambu’ alichokiimba katika mahadhi ya mduara.
Tale alisema, amevutika na kipaji hicho na hivyo ameona ni bora ampeleke studio kurekodi wimbo huo, ambao anaamini pindi utakapotoka utamtambulisha vema na pia kumweka katika nafasi za juu katika muziki.
“Nimeishafanya naye mazungumzo ya awali na muda si mrefu nitamuunganisha katika studio za Sound Crafters ili akarekodi singo yake,” alisema Tale.
Katika mahafali hayo, wahitimu pamoja na wasanii wengine waliopitia THT, walitoa burudani ya aina yake ambayo ilidhihirisha vipaji vya hali ya juu walivyonavyo.
Baadhi ya wasanii ambao wamepitia THT ni pamoja na Mwasiti Almas, Marlaw, Vumilia, Maunda Zorro, Barnabas, Mataluma, Amini, Linah na wengineo wengi

Comments