TASWA YATOA TAMKO KUHUSU KITENDO CHA TFF KUWABAGUA WAANDISHI WA MICHEZO KATIKA MECHI KUBWA

AMIR MHANDO, KATIBU MKUU WA TASWA
LEO Ijumaa Oktoba 8, wahariri 37 wa habari za michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari walikutana mgahawa wa Hadee’s jijini Dar es Salaam kuzungumzia masuala ya uingiaji wa waandishi wa habari kwenye mchezo wa kesho kati ya Taifa Stars na Morocco.
Kama tunavyofahamu ni kuwa TFF imetangaza kwamba itatoa tiketi maalum mchezo wa Taifa Stars na Morocco, badala ya kadi ambazo zimekuwa zikitumika katika michezo mbalimbali ya ligi.

Kutokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wanahabari za michezo kupinga uamuzi huo wa TFF, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kiliitisha mkutano na wahariri wa habari za michezo.

Mambo mbalimbali yalizungumzwa, huku malalamiko yakiwa mengi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linawanyanyasa waandishi wa habari na kuwatumia pale tu linapokuwa na maslahi yake.

Msimamo wa kikao ni kuwa kadi za TFF zinazotumika kwenye michezo mbalimbali si nyingi kama wengi wanavyodhania, na kwamba ingawa TFF inasema ilitoa kadi 170 mwaka 2008, idadi halisi ya wanaofanya kazi hiyo hawafikii hata 100.

Kwa misingi hiyo wajumbe wa kikao walikubaliana kwamba TFF itamke kuwa waandishi wa habari za michezo waruhusiwe kutumia kadi hizo kwa sababu wapo wanaoenda kwenye mechi kwa ajili ya kuripoti mpira, wengine kuandika makala, wengine kupiga picha na wengine matukio ya kawaida yasiyohusiana na mchezo wa uwanjani.

Mjumbe mwalikwa wa kikao hicho, Florian Kaijage ambaye ni Ofisa Habari wa TFF, alipopewa nafasi ya kuzungumza aliwaeleza wahariri kuwa tayari utaratibu uliokuwa umepangwa ni kuwa hakuna atakayepita mlangoni bila kuwa na tiketi.

Hivyo aliwaeleza wajumbe hata kama watakubaliana zitumike kadi, italeta vurugu kwenye majukwaa kwa sababu tiketi zina namba za viti.
Kaijage alipewa fursa ya kusikiliza hoja mbalimbali na mwishoni aliombwa na kikao aendelee na shughuli zake, lakini msimamo ukiwa wahariri wanataka zitumike kadi na si vinginevyo.

Hata hivyo baada ya majadiliano ya muda mrefu, kujali utaifa pamoja na busara za kiuhariri tulikubaliana yafuatayo:

(1) Kwa kuwa TASWA na Wahariri wanaamini TFF imekuwa ikifaidika zaidi na vyombo vya habari kwa kuandikiwa habari zao nyingi ambazo nyingine ni promosheni, kuna haja ikawathamini katika hili.

(2) TASWA na Wahariri wanaamini kwa kuwa idadi ya waandishi wanakaoingia uwanjani ni chache tofauti na wengi wanavyofikiri, na pia wengi wa waliopewa kadi mwaka 2008 hivi sasa karibu 50 hawapo kwenye vyombo vya habari na TFF haina haja ya kuogopa hilo.

Lakini kwa sababu TFF inasema ukaaji uwanjani utahusu namba za viti, basi TFF itenge tiketi 120 kwa ajili ya wanahabari.

Tiketi hizo zitasimamiwa na Ofisa Habari wa TFF kwa kushirikiana wa Wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, ambao ni Mhazini Sultani Sikilo na Mjumbe Grace Hoka.
Hawa watazigawa tiketi hizo kwa wote watakaokuwa na kadi za TFF za kuingia uwanjani zilizotolewa mwaka 2008.

Hivyo kitakachofanyika ni kwa mhusika kuonesha kadi yake ya TFF atapewa tiketi ya Taifa Stars na Morocco ili aingie uwanjani.
Hili litasaidia pia kudhibiti wale ambao hawapo kwenye vyombo vya habari, lakini wanamiliki vitambulisho, pia kuwa na uhakika wa namba halisi ya wenye vitambulisho badala ya hiyo ya TFF ambayo inaonekana si sahihi.

Hivyo kama hilo litakubaliwa waandishi wa habari za michezo wataombwa kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa 6 mchama wafike ofisi za TFF Uwanja wa Karume, Dar es Salaam ili wapewe tiketi lakini kwanza waoneshe hizo kadi za TFF.
(4)Viongozi wa TASWA wawasiliane na TFF wawaeleze msimamo huu na kama itatokea wenye kadi wakazidi idadi ya tiketi, hilo litafanyiwa kazi na busara itatumika kati ya TASWA na TFF ili kila anayestahili aweze kufika uwanjani.


Hata hivyo angalizo la wahariri ni kuwa wale ambao wanaelewa hawapo kwenye vyombo vya habari kwa sasa, hata kama wanazo kadi za kuingia uwanjani, wasiende maana hawatapewa tiketi na badala yake kadi zao zitazuiwa.
MSIMAMO:
Kama TFF ikishindwa kutekeleza hayo mapendekezo basi yafuatayo yatafanyika:

(1)Tiketi 70 ilizopanga TFF kutoa kwa ajili ya wanahabari hazitachukuliwa na mwandishi yeyote, badala yake TFF wazitumie wenyewe kadri watakavyoona inafaa wenyewe.

2)Vyombo vya habari vigharamie watu wake kwenda kuripoti mechi hiyo, bila kujihusisha kwa namna yoyote na TFF.

(3)Waandishi wa habari hawatajihusisha na kuandika habari za TFF zinahusu promosheni ya aina yoyote, isipokuwa habari ambazo ni za maslahi kwa Taifa ikiwemo mechi za timu za Taifa.Lakini masuala mengine ya TFF, ikiwemo kutangaza viingilio, adhabu za waamuzi ama hata kupata udhamini wa kitu fulani, wahariri wamekubaliana kwamba hilo halitafanywa.

Pia hata upigaji picha viwanjani katika maeneo ambayo ni kuitangaza TFF hayo hayatapewa nafasi.

Masuala mengine muhimu juu ya nini kifanyike wahariri wamekubaliana tena wakutane Jumatano wiki ijayo kujadili tena mambo mengine ya kufanya, ikiwa ni pamoja na utaratibu mzuri wa waandishi kuingia uwanjani na kufanya kazi zao bila bugudha.

Karibu vyombo vyote vya habari vilishiriki kwenye mkutano huo, ambao wengi waliupongeza uongozi wa TASWA kwamba ni mwanzo mzuri.

Mhando
Katibu Mkuu TASWA

Comments