TAMASHA LA 'REGGAE NITE TRIBUTE TO LUCKY DUBE' KURINDIMA OKTOBA 16, MSASANI BEACH

BAADHI YA WARATIBU WA TAMASSHA HILO KUTOKA KUSHOTO NI RAS JESHI,  RAS GWANDUMI, RAS BUMIJA NA RAS MIZIZI

TAMASHA maalumu la muziki wa reggae nchini linalojulikana kama ‘Reggae Nite Tribute to Lucky Dube’ litakaloambatana na kuliombea taifa amani katika kuelekea Uchaguzi Mkuu linatarajiwa kurindima Oktoba 16 Msasani Club jijini Dar es Salaam.

Tamasha hilo ambalo mbali ya kuliombea taifa amani siku hiyo, pia itakuwa kumbukumbu ya mwanaraggae maarufu barani Afrika, Lucy Dube na utambulisho wa albamu ya Ras Gwandumi inayokwenda kwa jina la ‘Raggae Bongo Dread’, limeandaliwa na taasisi ya Tanzania Rastafari Movement.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa Tanzania Rastafari Movement, Ras Jeshi Beku, alisema tamasha hilo ni maalumu kwa ajili ya kuombea amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, uzinduzi wa albamu ya ‘Bongo Raggae’ ya Ras Gwandumi wa Machifu Band.
Beku alisema, siku hiyo Jumamosi Oktoba 16, tamasha hilo litaanza majira ya saa 1:00 jioni na kuendelea hadi majogoo, huku likipambwa na Machifu Band na Ras Gwandumi, Jikho Manyika, Ras Mizizi na mwanadada Carola Kinasha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Paulo Alfred ‘Ras Bumija Zinyangwa’ aliwataka mashabiki wa burudani na wadau kwa ujumla kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuungana kuombea uchaguzi mwema, huru na haki, pia upite kwa amani, ili hata yale yanayotabiriwa kama kuwepo vifo na kutofanyika mwaka huu yasitokee.
Naye Kiongozi wa Machifu Band inayofanya kazi na Tanzania Rastafari Movement, Ras Gwandumi Kaisi alisema katika onyesho hilo mbali ya kutakia uchaguzi mwema, pia itakuwa ni kumbukumbu ya mwanamuziki wa reggae maarufu wa Afrika Kusini, Lucky Dube, aliyefariki Oktoba 19, 2007, pia atatambulisha albamu yake ya ‘Reggae Bongo Dread’.
Alisema, albamu hiyo itakuwa na nyimbo 16 zikiwamo ‘Ndoto’, ‘Nira’, ‘Ndugu Zetu’ ambao inapiga vita mauaji ya albino na uchunaji wa ngozi, ‘Lucky Dube’ maalumu kwa ajili ya kumuenzi msanii huyo na ‘Asante Jah’.
Nyingine ni ‘More Herbs’, ‘We Praise’, ‘Muziki wa Ras’, ‘Sweet Fields’, ‘Check Out’, ‘Simulizi ya Bibi’, ‘Jah Messiah’, ‘Sister Fire’, ‘Kupwa na Kujaa’, ‘Awake’ na ‘Tabasamu lake’, ukiwa mahsusi kumkumbuka aliyekuwa mwanareggae mahiri hapa nchini, Justine Kalikawe.
Ras Mizizi ambaye naye atashiriki katika tamasha hilo, alitanabaisha kuwa amejiandaa kufanya kweli siku hiyo.
“Nimejiandaa vizuri kuwaaamsha wenzangu na kuwakumbusha nyakati za Azimio la Arusha, Ujamaa na Kujitegemea, nitatoa zawadi maalumu ya vibao kama ‘Rastafari ndiyo njia yetu’, ‘Kitu cha Arusha’, na nyingine nyingi zikiwamo mpya zenye mtazamo wa kiroho, kimwili na kiakili katika ukombozi wa Mwafrika,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Tanzania Rastafari Movement, imemuonya Jackson Solomon, anayejulikana kama Ramking Boy, kuacha ubinafsi katika shughuli za taasisi na kuongeza kuwa ahusiki katika tamasha hilo, tofauti na alivyonukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni.
Pia walipinga kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kuwa reggae ni muziki ulioko ICU, bali uko juu ni wa heshima na wapenda amani duniani kote.

Comments