SIMBA YAING'OA YANGA KILELENI

KIKOSI CHA SIMBA
TIMU ya Yanga jana iliendelea kupunguzwa kasi katika mbio za kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.

Licha ya kila timu kucheza kwa juhudi kubwa, lakini Azam FC ambao walikuwa wenyeji wa mechi ya jana walionekana kutawala na kufanya mashambulizi mengi hasa katika kipindi cha kwanza.
Pamoja na hali hiyo, hadi mwamuzi Alinus Luena kutoka Mwanza anapuliza filimbi ya mapumziko, kulikuwa hakuna bao na katika kipindi cha pili, kila timu ilirejea dimbani kwa nguvu na kuendelea kushambuliana.
Katika dakika ya 72, Azam FC nusura wapate bao, lakini shuti kali la Jamal Mnyate aliyekuwa ameingia dakika ya 64 badala ya Selemani Kassim, liliokolewa na kipa wa Yanga, Yaw Berko.
Hiyo ni sare ya pili mfululizo kwa Yanga, kwani katika mechi iliyopita, vijana hao wa Kocha Kostadin Papic walivuna matokeo kama hayo kwa maafande wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 21, hivyo kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo huku Simba ambayo jana iliifunga JKT Ruvu mabao 2-1, ikitwaa usukani wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 21.
Licha ya Simba kuwa na pointi 21 kama ilivyo kwa mtani wake Yanga, lakini yenyewe imefunga mabao 14; Yanga wakifumania nyavu mara 10 huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Azam FC yenye pointi 14.
Katika mechi ya Simba iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Simba ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 28, likifungwa na Rashid Gumbo.
Gumbo alifunga bao hilo kwa shuti kali la nje ya maguu 18, akiifanyia kazi pasi maridadi ya Jerry Santo, hivyo kuamsha kasi ya JKT Ruvu, lakini safu ya ulinzi ya Simba nayo ikiwa makini.
Dakika ya 44, Simba walipata bao la pili, safari hii likifungwa na nyota wake wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, baada ya kupata pasi ya Haruna Shamte na kuukwamisha mpira wavuni.
Licha ya JKT Ruvu kupambana vilivyo kukomboa mabao hayo, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, walikuwa mbele kwa mabao hayo mawili.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa cha kasi zaidi kwa JKT Ruvu kuonekana kucharuka zaidi na juhudi hizo kuzaa matunda katika dakika ya 80, baada ya kupata bao likifungwa na Hussein Bunu akipokea pasi ya Abdallah Bunu.

Comments