MISS PROGRESS INTERNATIONAL KUSAIDIA MAPAMBANO DHIDI YA MAUAJI YA MAALBINO

Katibu Mtendaji wa BASATA Bw.Materego akisisitiza jambo  kwenye Jukwaa la Sanaa ambapo alimpongeza Julieth kwa mpango wake wa kupambana na mauaji dhidi ya maalbino, kushoto kwake ni mshindi wa taji la Miss Progress International Julieth William.

Mshindi wa Shindano la Urembo la Progress International Julieth William amesema kwamba waandaaji wa shindano hilo lililofanyika nchini Italia hivi karibuni na kushirikisha warembo zaidi ya 50 kutoka mataifa mbalimbali wamemtengea kitita cha Euro 20,000 sawa na shilingi milioni 40 za kitanzania kwa ajili ya kupambana na mauaji dhidi ya walemavu wa ngozi (maalbino)

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii,Julieth alisema kwamba, fedha hizo amezipata kufuatia kuandika andiko la mradi (proposal) la jinsi ya kupambana na mauaji ya walemavu wa ngozi ambalo lilimpa asilimia 50 za ushindi kwenye shindano hilo.
Alisema kwamba, anasikitishwa na kuumizwa na mauaji dhidi ya binadamu wasio na hatia na kusisitiza kwamba,lazima watanzania wabadilike na kujua kwamba utajiri au mafanikio katika shughuli zao hayapatikani kutokana na viungo vya binadamu bali juhudi katika kazi na kujituma.
Alisema kwamba, mradi wake huo ambao atauendesha kwa kushirikiana na wanaharakati wengine utajikita kwenye maeneo ya kanda ya ziwa ambapo atakuwa akitoa elimu kwa umma,uhamasishaji wa jamii dhidi ya vitendo hivyo, kuunda Kamati ndogondogo chini ya walemavu wa ngozi zitakazokuwa zikifanya kazi ya kuielimisha jamii na mambo mengine mengi.
Aliongeza kwamba,ameshaanza mazungumzo na serikali ili kuona ni kwa jinsi gani atashirikiana nayo katika kufanikisha mradi huo ambao alisema kwa kuanzia utalenga maeneo yaliyoathirika zaidi ambayo ni ya Mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Kuhusu ushindi wake kwenye Shindano hilo la Miss Progress International ambapo aliwabwaga warembo zaidi ya 50 kutoka nchi mbalimbali, alisema ulitokana na yeye kutokukata tamaa,kujenga utamaduni wa kutafuta fursa na kuzitumia ipasavyo,kujituma na kujiamini.
Aliwaasa warembo kutokubweteka na kukata tamaa bali kujenga utamaduni wa kujiamini,kusaka fursa mpya na kuzitumia ipasavyo, kuwa mfano katika jamii kwa kuwa na maadili bora na zaidi kujihusisha na masuala mbalimabali ya kijamii.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alimpongeza Julieth William kwa ushindi wake zaidi wazo lake la kushirikiki vita dhidi ya mauaji ya walemavu wa ngozi na kumueleza kwamba BASATA iko pamoja naye kwani ni mlezi wake.
Alisema kwamba, warembo hawana budi kujifunza kutoka kwenye mafanikio ya Julieth kwani kwa muda mrefu Tanzania pamoja na kupeleka warembo kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa wamekuwa hawafanyi vizuri sana ingawa alisema wamekuwa wakiitangaza nchi kwa kiwango kikubwa.
Wachangiaji wengi kwenye Jukwaa la Sanaa walimpongeza Julieth na kumtakia kila la kheri kwenye mradi wake huo ingawa pia hawakusita kumuonya dhidi ya tabia zisizofaa ambazo zimekuwa zikioneshwa na warembo mara wanapopata mafanikio.
ni mlezi wake.

Comments