HAKEEM 5:BAADA YA KUSOTA SASA ANAKULA RAHA KATIKA MUZIKI

HAKEEM 5
LICHA ya kuanza kujihusisha na masuala ya muziki kwa muda mrefu, msanii anayekwenda kwa jina la HAKEEM 5 nyota yake ilishindwa kung’ara kama ilivyo sasa.
Kwa mashabiki hasa wa muziki wa kizazi kipya jina lake sio geni vichwani mwao kwani kazi zake ambazo hazikumpatia umaarufu sana zilikuwa zikisikikia katika baadhi ya vituo vya reduio.
Kama hiyio haitoshi, kwa wale vijana waliokuwa wakihudhuria matamasha mbalimbali walikuwa wanabahatika kuona makamuzi yake jukwaani ambapo kwa hakika walikuwa wakiamini siku moja atakuwa msanii mwenye jina.
Mungu si athumani kwani kwa sasa Hashim Hashim Masokelo maarufu kama ‘Hakeem 5’ nyota yake imeweza kung’aa na hivyo kufanikiwa kuingia katika orodha ya wasanii wanaotesa kwa sasa.
Akizungumza katika mahojiano na Sayari juzi Hakeem 5 anasema hatobweteka na kiwango alichofikia bali atakaza buti ili kuweza kushika chati za muziki huo huo ulioliteka soko la muziki nchini.
Anasema kubwa ni kujibidiisha katika kutayarisha kazi na pia kuimba nyimbo ambazo hazipitwi na wakati na mwisho wa siku mashabiki watakuwa wakikubali kazi zako hata ziwe na muda mrefu kiasi gani.
Anaongeza kuwa, hata ushindani uliopo katika soko la muziki wa bongo fleva ni mkubwa sana hivyo ni muhimu kuumiza kichwa na kuandaa kazi nzuri.
“Unajua muziki huu umekuwa na ushindani mkubwa na hasa ikizingatiwa kuibuka kwa wasani wapya wazuri kila kukicha, bila kufanya jitihada unaweza ukajikuta unapotea kabisa”, Anasema.
Hata hivyo haikuwa rahisi kwa mzsanii huyo kufikia hapo alipo kwani alikumbatana matatizo mengi katika harakati za kusaka kutoka, pia kuingia studio kwa ajili ya kurekodi kazi zake haikuwa jambo jepesi.
“Namshukuru mungu kwa kiwango nilichofikia kwani nilipoanza muziki watu walikuwa wakinidharau, lakini sikukata tamaa na niliendelea jitihada zangu na mpaka kufikia hapa nilipo”, Alisema Hakeem.

Historia yake kimuziki:
Hakeem 5, jina linalotokana na majina ya ndugu zake waliozaliwa tumbo moja H-ashim, A-dam, K-arol, E-Elizabeth na M-Musa.
Alianza kupenda muziki tangu alipokuwa mdogo na kadiri alipokuwa anakuwa mapenzi yake katuika muziki yalikuwa yakiongezeka kadiri siku zinapoongezeka, huku akiimba zaidi nyimbio za kukopi toka kwa wasanii wengine.
Akiwa shule ya Msingi alishawishiwa kuimba muziki na mmoja ya watu wake wa karibu anayekwenda kwa jina la Mudy ambaye alikuwa ni muimbaji mzuri kabla kukutana na O- Tesa ambaye alianza kumfundisha kiundani zaidi,
Zamani alikuwa akipenda zaidi muziki wa bolingo lakini alipoanza kufanya muziki kama kazi yake ndipo alipoanza kuimba muziki wa kizazi kipya.
Mapenzi yake katika muziki yalimfanya akatize masomo yake ya sekondari katika sekondari ya Jitegemee alipokuwa kidato cha pili ili aweze kufanya kitu ambachoroho yake inapenda.
“Kipindi ninasoma nilitoa wimbo wangu wa kwanza mwaka 2004 ‘Anapendeza’ hivyo walimu na wazazi wangu walikuwa wakinisema sana, hivyo niliona ni bora niache shule kabisa nijikite katika muziki”, Alisema.
Baada ya kuacha shule alizidi kujika katika mambo ya muziki ambapo alikuwa akiimba katika matamasha mbalimbali na hivyo kuweza kupata fedha zilizomuwezesha kuingia studio na kurekodi baadhi ya kazi zake.
Mwaka 2007 aliingia studio za G- Records na kurekodi singo ya ‘Mapenzi Matamu’, kabla ya mwaka 2009 kurekodi singo ‘Namashaka na Wewe’ katika studio za Am akimshiruikisha Mr.Blue.
Aidha, Aprili mwaka 2010, Hakeem 5 aliachia singo yake ya nne inayokwenda kwa jina la ‘Oiyee’ ambapo kazi ya kurekodi ilifanywa pia studio za Am chini ya mtayarishaji Manek.
Kwa sasa Hakeem ameingiza sokoni albamu yake ya kwanza akienda kwa jina la ‘Namashaka na Wewe’ ambayo inabebwa na nyimbo kumi.
Nyimbo hizo ni pamoja na ule uliobeba jina la albamu ‘Namashaka’ ambao amemshirikisha Mr.Blue, ‘Oiyee’, ‘Nakukunda’ alioimba kwa lugha ya Kinyarwanda akimshirikisha Pasha, ‘Anapendeza’ aliomshirikisha Dully Sykes.
Pia zimo ‘Msela’, ‘Sio Vizuri’, ‘Friday’, ‘Mapenzi Matamu’, ‘Wivu Kila Saa’ na ‘African Girl’ huku nyimbo hizo zikirekodiwa katika studio za G Records, Am na Latino.
Hakeem anasema baada ya kuingiza sokoni albamu hiyo kwa sasa ameanza kuitangaza kupitia maonyesho anayopata kwenda kutumbuiza katiak miji tofautio nchini, hivyo amewaomba mashabiki wake kununua kazi zake.
Akiwa na matarajio ya kufika mbali katika muziki huo, Hakeem anawashauri wasanii wenzake kuheshimu kazi zao, pia kutobweteka na mafanikio waliyonayo bali wanatakiwa wajitume kwa nguvu zote.
Mkali huyo ambaye alipanda chati zaidi aliposhirikishwa na Ali Kiba katika singo ya ‘Nakshi Mrembo’ anavutiwa zaidi na kazi za Belle 9.

Comments