ESTHER FLAVIAN:NYOTA MPYA WA FILAMU ZA KIBONGO ASIYEVUTIWA NA WAIGIZAJI WA KIKE WA HAPA NCHINI

ESTHER FLAVIAN

ESTHER KATIKA POZI
KUKUA kwa tasnia ya filamu nchini kunakwenda sambamba na kuongezeka kwa ushindani baina ya wasanii kwa wasanii kila kukicha, na hilo linatokana na kuibuka kwa wasanii wapya wanaokuja na vipaji vya hali ya juu, hivyo kuwapa changamoto wasanii waliowatangulia kwenye fani hiyo.


Hali hiyo imesababisha wasanii waliopo kwa muda mrefu kuumiza vichwa kwa kufanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu ili kuweza kukamata chati za wasanii wanaofanya vema.

Esther Flavian Mushi ni miongoni mwa wa wasanii walioanza kuonyesha cheche zao katika tasnia hiyo siku za karibuni na tayari ametabiriwa kuwa nyota wa fani hiyo baadaye.

Muonekano huo unatokana na filamu chache alizoigiza tangu ajitose katika medani hiyo kufanya vema katika eneo alilopangwa, na hasa kuuvaa vyema uhusika.

Kama hiyo haitoshi, Esther ana mvuto wa kike hasa unaokubalika kwa mashabiki wa filamu, hali inayochangia pia kazi zake kuonekana nzuri zaidi hivyo kujiongezea mashabiki.

Kwa haraka haraka Esther ameshacheza filamu kama tano hivi ambazo kwa hakika ameweza kudhihirisha uwezo wa hali ya juu alionao katika kazi hiyo.

Msanii huyo anasema alianza kuipenda fani hiyo tangu akiwa mdogo, lakini pindi alipofikia usichana alianza kuvutiwa zaidi na waigizaji wa kike wa nchini Nigeria.

“Kwa kweli wasanii kutoka Nigeria kama Rita Dominic, Genevieve Nnanji, Omotola ndio walikuwa wakinivutia sasa, na hivyo nilipokuwa nikiangalia kazi zao nilikuwa napanga nguvu na msukumo wa kutaka na mimi siku moja niwe kama wale na ikiwezekana niwazidi,” anasema.

Hata hivyo, Esther ni mmoja ya wasanii wenye mitazamo tofauti na wengine kwani kwa upande wake anasema havutiwi na muigizaji yeyote wa kike hapa nchini, ila kwa upande wa wanaume anavutiwa zaidi na Steven Kanumba.

“Yaani sijaona msanii wa kike anayeigiza vizuri, wote wapo kawaida sana, lakini kwa wanaume Kanumba ni moto wa kuotea mbali, kwanza ana kipaji cha asili, na ni msanii ambaye amejitosheleza kila idara katika kazi zake, hivyo hata ukiangalia kazi zake huwezi kuchoka,” anasema.

Anaongeza kuwa kutokana na umahiri alionao, atajisikia furaha kubwa iwapo siku moja atapata nafasi ya kucheza filamu na mkali huyo kwani anaamini itakuwa bomba, na pia itaweka historia.

Mwaka 2008 ndipo alipoanza rasmi kazi ya kucheza filamu na kipindi hicho alikuwa mwanafunzi katika chuo kimoja jijini Dar es Salaam, na alijiunga na Kampuni ya D Production inayofanya kazi ya kutayarisha filamu na kazi nyingine za sanaa.

Anasema taratibu alianza kufanya mazoezi nyumbani, na hata aliposhirikishwa kuigiza filamu ya kwanza (Its Too Late) akicheza kama mpenzi wa Yussuf Mlela akitumia jina la ‘Alice’ haikumpa tabu sana kuuvaa uhusika.

Baada ya Its Too Late ndiyo ikawa mwanzo wa Esther kushirikishwa katika filamu nyingine. Mwaka 2009 alicheza Where is Love, na baadaye Zawadi ya Operation na Fake Pregnant.

“Pa nimeshiriki kama kinara wa filamu ya Aunt Suzzy ambayo ipo mbioni kutoka wakati wowote, humo ndiyo nimeharibu mbaya, hivyo nawaomba mashabiki wa filamu za Kibongo kukaa tayari kuinunua ili kuweza kupata burudani safi,” anasema.

Akizungumzia ushindani uliopo katika tasnia hiyo, anasema anajiamini kuwa ana kipaji pamoja na uwezo mkubwa ambao utawezesha kazi zake kubamba ipasavyo na hivyo kuliteka soko.

“Kama nilivyokwambia, mimi ninajiamini na nimejipanga kikamilifu katika mambo ya uigizaji, pia simuhofii msanii yeyote wa kike kama wengine wanavyoogopana, yeyote atakayepata nafasi ya kushirikishwa na mimi nitamfunika vibaya sana,” anasema.

Kuhusu rushwa ya ngono katika fani hiyo, msanii huyo anakiri kuwa mchezo huo upo, lakini inategemea na tabia ya msanii mwenyewe, kama atakubali kujidhalilisha kwa kuwavulia nguo waongozaji ni juu yake.

“Suala la ngono lipo na mimi nilishawahi kukimbia kufanya kazi na mtu fulani ambaye alikuwa anataka nimpe ngono ili niweze kutoka katika filamu yake, kwa kweli hiki kitu si kizuri kwani hakitakuza sanaa bali kinadidimiza, pia msanii unatakiwa ujue nini unafanya,” anasema.

Akienda mbali zaidi, Esther anasema amedhamiria kufika mbali katika fani hiyo na moja ya malengo yake ni kucheza filamu sambamba na mmoja wa nyota wa Nigeria ambako anaamini huko wamepiga hatua kubwa katika fani hiyo kwa bara la Afrika.

Akizungumzia matatizo anayokumbana nayo katika kazi zake, anasema yapo mengi, lakini kubwa ni usumbufu kutoka kwa wanaume wakware ambao imekuwa ni kawaida yao kusumbua wasichana, pia kudhulumiwa ujira wake baada ya kufanya kazi ambayo imemgharimu pesa nyingi.

“Kwa kweli dada yangu si mimi tu, hata wasanii wengine wa kike tunasumbuliwa sana na wanaume wakware. Lakini kwa vile nina msimamo wangu mwenyewe, ninawapotezea na kuendelea na kazi. Lakini tatizo jingine ni kudhulumiwa ujira wako, mfano mtu umecheza filamu na kujigharamia baadhi ya mahitaji, lakini mwisho wa siku mtayarishaji kukulipa inakuwa tabu,” anasema.

Kwa mantiki hiyo amewashauri watayarishaji wenye tabia za kudhulumu malipo ya wasanii kuacha tamaa ya kutaka kitu ambacho hawana uwezo nacho. “Kama unataka kufanya biashara ya filamu lazima uwe na pesa ya kuwalipa wasanii, sio wanataka mambo makubwa halafu wakishamaliza kututumia kwenye kazi zao wanashindwa kutulipa, hiyo haipendezi,” anaongeza.

Esther ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya wawili wa mama Rosemary Kiondo na baba Flavian Mushi, alizaliwa Juni 5, 1989 mjini Tanga na kusoma katika Shule ya Msingi Mission huko Tanga kati ya mwaka 1996 hadi 2002 na kisha kujiunga na Sekondari ya GTI jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 2003 hadi 2006. Baada ya hapo alijiendeleza kwa kozi za kompyuta na ukatibu muhtasi katika vyuo tofauti.

Comments