DAV D:TUNDA JINGINE LA THT, ANATAMBA NA SINGO YA ZINDA

DAV D
MUZIKI wa kizazi kipya umekuwa na ushindani kila kukicha, hilo linatokana na kuibuka kwa wasanii wenye vipaji vya hali ya juu.
Kama hiyo haitoshi, wasanii hao wapya pamoja na vipaji pia wamekuwa wakitoa nyimbo nzuri zinazowaweka katika nafasi za juu katika chati mbalimbali.
David Richard Mataula maarufu kama ‘Dav D’ ni mmoja ya wasanii ambao wamefanikiwa kuingia katika orodha ya wasanii wenye uwezo wa hali ya juu.Dav D ambaye ni mwanafunzi katika kituo cha Nyumba ya vipaji Tanzania (THT) umahiri alionao unaleta picha ya kwamba atakuwa mmoja ya wasanii watakaoleta ushindani mkubwa katika siku zijazo.
Kwa mantiki hiyo Dav D anaingia katika orodha ya wakali wa sasa chipukizi akiungana na kina Barnaba, Amin, Sam wa Ukweli, Mataluma, Linah, Diamond, Samir na wengine wengi.
Licha ya kuwa jina lake siyo maarufu sana masikioni mwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini, lakini kibao chake kijulikanacho kama ‘Zinda’ ndicho chenye umaarufu mkubwa.
Kibao hicho ambacho ni cha kwanza kwake alikirekodi katikati ya mwaka huu katika studio za Soundcrafters chini ya mtayarishaji wake, Henrico.
Baada ya kuvuma kwa kibao hicho katika vituo vya redio mbalimbali hapa nchini, sasa hivi yupo mbioni kuanza kurekodi video ya wimbo huo.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii, David D anasema pamoja na wimbo wake huo kuweza kukubalika lakini bado hajaridhika na mafanikio hayo, hivyo atahakikisha anafanya jitihada zaidi.
“Namshukuru mungu nimetoa kazi ya kwanza imeweza kupokewa vizuri na mashabiki inagawa si kwa kiasi kikubwa lakini ni mwanzo mzuri na imenipa mwanga fulani na nguvu ya kujipanga zaidi”, Anasema.
Anaongeza kwa kusema kuwa kutokana na mafunzo aliyoyapata na anayoendelea kuyapa THT anaamini yatamuwezesha kufika mbali zaidi katika medani ya muziki ambayo ameamua iwe ni sehemu ya kazi yake.
Anaongeza kuwa kutokana na ushindani mkubwa uliopo katika tasnia ya muziki bila ubunifu wa hali ya juu na kutoa nyimbo zenye ujumbe mzito kwa jamii itakuwa ni ngumu kupenya mafanikio.
“Hii kazi si lelemama kama watu wanaovyoona, ili upate nafasi ya kukubalika inabidi utumie ubunifui pamoja na mashairi yenye maana, kinyume na hapo nyimbo zako zitaishia kupigwa kwenye kumbi za starehe tu”, Anasema.
Dav D anasema yupo mbioni kuingia studio kwa ajili ya kutayarisha albamu yake ya kwanza ambapo kama mambo yataenda vizuri itakamilka mapema mwakani.
Anasema albamu hiyo atairekodi katika studio tofauti, pia akitarajia kuwashirikisha wasanii kama Banana Zoro, Linah, Mataluma na Barnaba.
“Ninataka nitoke na albamu ambayo itakuwa na ladha, pamoja na mitindo tofauti ili kuweza kuwashika mashabiki wa aina zote”, Anasema.
Akizungumzia matatizo anayokumbana nayo katika kazi zake, Dav D anasema kubwa ni usumbufu wa kupata nafasi ya kuingia studio na hasa kwa wasanii wanaochipukia.
Akiwa na matarajio ya kufika mbali zaidi sambamba na kumiliki bendi, Dav D anawashauri wasanii wenzake kutoridhika na mafanikio madogo wanayoyapata bali wajitume sana ili wafanikiwe zaidi.
Dav D, alizaliwa Septemba 26, 1990 Mvomero, Morogoro na kupata elimu ya Msingi katika shule ya Mazoezi iliyopo Mvomero kati ya mwaka 1997-2002, kabla ya kujiunga na sekondari ya Lusanga iliyopo Mtibwa, Morogoro aliposoma mwaka 2003 – 2006.
Alianza kuupenda muziki tangu akiwa mdogo, kabla ya mwaka 2008 kujiunga na THT ambapo anaendelea kujifunza mpaka sasa, huku pia akiwa na uwezo wa kupiga baadhi ya vyombo vya muziki.

Comments