WATEJA WA VODACOM KUNEEMEKA ZAIDI

Dar es Salaam, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imezindua programu mpya ya Tuzo Pointi ambayo itawawezesha wateja wake kupata punguzo kubwa la bei wakati wakipata huduma katika sehemu mablimbali kama mahotelini, ofisi za bima na madukani.
Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Wateja, Aika Matiku alisema kwamba huduma hiyo itawawezesha wateja wake kupata punguzo la kati ya asilimia 5 hadi 20 kutoka kwa wauzaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini.
Aliwataja baadhi ya watoaji wa huduma ambao wataanza nao kuwa ni duka la Woolworth, Sunrise Beach Resort na kampuni ya Bima ya Real Insurance. Hoteli za Kunduchi Beach Resort na Zanzibar Beach Resort zitaanza kutoa huduma baada ya kukamilisha taratibu.
Alisema wateja wanaoweza kupata punguzo hilo kubwa ni wale wenye pointi 250 za Tuzo na kuendelea.
“Tumeanzisha huduma hii kwa lengo la kuhakikisha kwamba wateja wetu wanapata huduma bora na kwa bei nafuu,” alisema.
Alisema huduma hiyo ni sehemu ya programu ya Tuzo Pointi ambayo lengo lake ni kuwazawadia wateja wake waaminifu na kuboresha maisha ya wateja wake.
Alisema mteja anapata pointi kwa njia kuu tatu. Moja ni kwa utumiaji ambapo wateja wa malipo ya kabla watakapotumiaSh 100 na wale wa malipo ya baada watakapotumia Sh 500 wote watapata pointi moja ya Tuzo.
Njia ya pili ni kwa kuongea, akifafanua njia hii alisema mteja akipokea simu kutoka mtandao mwingine atapata pointi moja ya Tuzo.
Njia ya tatu ni ile ya mteja wa Vodacom atakapoendelea kuwa mteja wa Vodacom kwa wiki moja huku akitumia simu yake kwa kupokea simu, kupiga, kutuma ujumbe wa maneno au kupokea ujumbe wa maneno atapata pointi nyingine moja ya Tuzo.
Alisema kwa wateja wa mikoani wataweza kupata huduma wakiwa huko huko kutoka kwa vituo mbalimbali vya huduma na maduka vilivyoko mikoani.

Comments