UCHAGUZI TEFA TAFRAN, AL MANUSRA NDOLANGA ACHEZEE KICHAPO

MWENYEKITI WA CHAMA CVHA SOKA MKOA WA DAR ES SALAAM (DRFA) ALHAJ MUHIDIN NDOLANGA

MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Alhaji Muhidin Ndolanga, amenusurika  kupigwa na wapambe wa wagombea watatu walioenguliwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (TEFA).


Wapambe wa wagombea hao walivamia Ofisi za (DRFA) majira ya saa sita mchana na kumtaka Ndolanga kuwarejesha katika kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa madai kuwa Kamati ya Uchaguzi ya (TEFA) haikuwatendea haki kuwaengua na kwamba wana vigezo vya kushiriki uchaguzi huo.
Walioenguliwa katika uchaguzi ni Abdulhabib Abdalah, aliyekuwa anawania nafasi ya mwenyekiti, Azizi Mohamed, makamu wa kwanza wa mwenyekiti na Omari Abdulkadir, nafasi ya ujumbe wa mkoa.
Akithibitisha kutokea kwa vurugu hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya (DRFA), Alhaji Muhidini Ndolanga, alisema wagombea hao walivamia ofisi hizo na kufanya vurugu kwa kumtishia huku wakigonga meza za ofisi hiyo ili kumshinikiza awarejeshe katika uchaguzi huo ambao umepangwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa JKT Mgulani.
Alisema maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi kuwaengua wagombea hao yatabakia pale pale na kusisitiza kufanyika kwa uchaguzi huo kama ilivyokwisha kupangwa.
Ndolanga, mwenyekiti wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT) alisema tayari tukio hilo limesharipotiwa Kituo cha Polisi Msimbazi na kupewa RB; MS/RB10208/2010 kwa ajili ya Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa vurugu hizo.
Wagombea wanaochuana katika kinyang’anyiro hicho kwa upande wa mwenyekiti ni Peter Mhinzi na Msanifu Kondo, Makamu wa kwanza wa mwenyekiti ni Meba Ramadhani na Saleh Mohamed huku Makamu wa pili wa mwenyekiti akiwa Bakili Makere, Juma Lunje na Siza Chenja.
Kwa upande wa ujumbe wa kuwakilisha mkoa ni Francis Peter, mweka hazina Abraham Barabara na Yusuf Kinega wakati mweka hazina msaidizi ni Heri Kaiza.
Wajumbe ni Albino Lwira, Fikiri Magoso, Hamis Balawa, Obby Steleki, Ally Kulita na Mfaume Ramadhani.

Comments

  1. Nakusawazisha Mwenyekiti wa DRFA ni Amin Bakhressa na si Muhidin Ndolanga. take care mama Ndolanga ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi

    ReplyDelete

Post a Comment