SIMBA YAPIGWA 3-1 NA GOR MAHIA




MABINGWA wa soka wa Ligi Kuu Bara, Simba, leo wamekiona cha moto baada ya kulimwa mabao 3-1 na Gor Mahia ya Kenya katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Gor Mahia, moja ya timu kongwe na maarufu nchini Kenya na Afrika Mashariki na Kati, iliwachukua dakika mbili tu kupata bao la kwanza likifungwa na Ochela Francis.
Wakionyesha kwa juhudi, ujuzi na stamina, vijana wa Gor Mahia walionekana kuwazidi Simba, kwani katika dakika ya 12, Ochela alirejea kwenye nyavu za Simba na kufunga bao la pili kwa timu yake, akimtungua kipa Ally Mustafa ‘Barthez.’
Licha ya Simba iliyo chini ya Kocha Mzambia, Patrick Phiri kucharuka kwa lengo la kusawazisha mabao hayo, ukuta wa Gor Mahia ulikuwa makini kuokoa hatari nyingi.
Dakika ya 20, Phiri aliamua kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne, lakini bado Simba walionekana kulemewa na vijana wa Kenya ambao walikuwa wakicheza soka ya kuvutia kwa dakika zote 90.
Juhudi za Gor Mahia zilidi kuzaa matunda katika dakika ya 43 pale Okoth Collins alipoifungia timu yake bao la tatu, hivyo Simba kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa kigumu kwa Simba kwani licha ya kupambana vilivyo kusawazisha mabao hayo, mabeki wa Gor Mahia walikuwa makini.
Dakika ya 90, Simba walifanya shambulizi la nguvu langoni mwa wapinzani wao na kutokea piga-nikupige, hivyo Amir Maftah akaifungia Simba bao la kufutia machozi.
Gor Mahia wapo nchini kwa ajili ya kucheza mechi mbili dhidi ya timu kongwe za Simba na Yanga, ambazo zimepumzika kwa muda kucheza Ligi Kuu kutokana na nyota wao wengi kuwa katika timu ya Taifa Stars.
Simba: Ally Mustapher, Haruna Shamte, Juma Jabu, David Naftar/ Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Abdulhalim Humoud, Rashid Gumbo/ Uhuru Selemani, Amri Kiemba/ Mohamed Banka, Mohamed Kijuso, Kevin Chale/ Emmanuel Okwi na Salum Aziz.
Gor Mahia: Kagunzi Ronnie, Nasio Solomon, Masika Eric, Wekesa Christopher, Mohammed Mussa, Akamu Anthony, Okoth Collins, Ngwa Baldin, Ochela Francis, Makori Dun na Opndo Cliff.

Comments

  1. Thanx alot kwa habari moto, mseto na kwa haraka
    Baraka kwako
    Nimekuona kwenye link za Prof Matondo na nimefarijika kutembelea hapa
    Baraka kwako

    ReplyDelete

Post a Comment