YANGA WANYIMWA KUTUMIA UWANJA WA TAIFA


SAKATA la kutumia Uwanja wa Taifa uliyoko Jijini Dar es Salaam kwa timu za Simba na Yanga, limechukua sura mpya baada ya Simba kubadili uwamuzi wa kwenda Mwanza na kutaka kubaki Jijini Dar eSalaam kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

Habari zilizopatikana jana jioni, zinasema kubadili mawazo huko kwa Simba kumepelekea Serikali kuinyima Yanga uwanja huo, licha ya kuwepo taarifa za kukubaliwa kuutumia.
Habari hizo, zinabainisha kwamba baada ya vikao vya siku kadhaa kati ya uongozi wa Yanga na serikali kuhusiana na uwanja huo, Yanga ilikubaliwa, lakini kitendo cha watani wao wa jadi kupelejka barua ya maombi kwa siri kimesababisha serikali kubadili uamuzi.
Hatua hiyo, inafuatia Uwanja wa Uhuru kufungwa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati , hali iliyosababisha timu hizo kongwe nchini kusaka viwanja kwa ajili ya michezo inayoikabili.
Awali serikali ilitoa masharti kadhaa ambayo yaliifanya Simba ibadili mawazo na kuamua kutanga kutumia uwanja wa CCM Kirumba uliyoko mkoani Mwanza.
Kutokana na hali hiyo, Yanga italazimika kuhamishia michezo yake kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Comments